Home »
» WAKAZI WA BUIGIRI WAISHUKURU SERIKALI KUWEKEWA MATUTA BARABARANI
WAKAZI WA BUIGIRI WAISHUKURU SERIKALI KUWEKEWA MATUTA BARABARANI
Na Peter Mkwavila CHAMWINO.
WANANCHI wa Kata ya Buigiri Wilaya Chamwino Mkoani Dodoma wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Barabarani (TANROAD) kwa kuwawekea matuta pamoja na alama za barabarani, hatua ambayo wamesema itasaidia kupunguza wimbi la ajali za mara kwa mara zilizokuwa zikitokea katika eneo hilo.
Wananchi hao wamesema kwa muda wa miaka nane, eneo hilo limekuwa likishuhudia ajali za mara kwa mara kutokana na ukosefu wa matatu ma alama za barabarani.
Wakizungumza Nipashe wananchi hao wameelezea kufurahishwa na hatua hiyo muhimu iliyofanywa na Serikali kupitia TANROAD.
Godwin Madeje, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Chamwino ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwajari wananchi, hususan wazee katika kata na nchi nzima kwa ujumla.
“Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiwapoteza wazee wenzetu wengi kupitia ajali za barabarani kutokana na kutokuwepo kwa alama za barabarani pamoja na matuta. Eneo letu la vijiji vitatu vya Buigiri,Chingali na Mwegamile linapitiwa na barabara ya Dodoma kwenda Morogoro inayotumiwa na magari mengi, pamoja na mabasi yanayokwenda kwa kasi sana, hali ambayo imekuwa ikiwapa changamoto kubwa sana wazee, wanafunzi, watu wenye ulemavu pamoja na watoto katika uvukaji,” alieleza.
Kwa upande wake, Michael Msuya, Mwalimu mstaafu, pamoja na kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na TANROAD, alisema ipo haja ya Serikali kuhakikisha jeshi la polisi linaweka mifumo endelevu ya kusimamia madereva, hususan wale wanaoendesha magari ya Serikali kupunguza mwendo pindi wanapopita katika maeneo yenye alama za barabarani na matuta.
Mchungaji Julias Chigo wa Kanisa la Angalikan Buigiri, alisema hatua iliyochukuliwa na serikali yakuweka matuta na alama za barabarani imewajali wananchi wa kata hiyo ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wakiomba alama hizo.
“Wananchi wa kata hii ya Buigiri walikuwa wakigongwa kama wanyama, hivyo tunamshukuru Rais wetu kwa kusikia kilio chetu na tunaamini sasa vifo vitapungua haasa kwa makundi ya watoto,wasioona,walemavu na wazee ambao walikuwa ni wahanga na ajali hizo”alisema.
Aidha, kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino, Keneth Yindi, alisema kuwa toka mwaka 2015 hadi 2022 wananchi wa kata ya Buigiri walikuwa na kilio cha kuiomba serikali kuwekewa matuta na alama za barabarani.
Alisema kilio hicho ni kutokana na wananchi wa eneo hilo kukutwa na majanga ya kugongwa mara kwa mara na kusababisha vifo na ulemavu wa kudumu kwa watu ikiwemo na uharibifu wa miundombinu iliyokuwa kando kando na barabara.
“Kuanzia mwaka 2016 nilikuwa ninaenda mara kwa mara wizarani kuomba kwenye kata yangu ambayo ipo kwenye barabara ya kutoka Dodoma kwenda Morogoro kuwekewa alama za barabarani ikiwemo matuta ili kunusuru maisha ya wakazi hasa kwenye maeneo yaliyopo shule maalum wasioona, kambi ya walemavu wasioona ya matembe bora”alisema.
Yindi ambaye ni diwani kuanzia mwaka 2016 wa kata hiyo ya Buigiri alisema kuwa kitendo cha kuwekewa kwa alama hizo za barabarabi ni hatua muhimu iliyodhihirisha namna ambayo serikali imewaheshimu wananchi wake.
Makamu Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wa kata hiyo kuhakikisha wanakuwa walinzi wa kuitunza miundombinu iliyowekwa huku wakiwa waangalifu wanapokuwa barabarani.
0 Comments:
Post a Comment