Subscribe Us

*NAIBU WAZIRI DKT. KIRUSWA AIHAKIKISHIA NCHI YA KOREA KUSINI FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI*

Na. Mwandishi wetu Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameihakikishia Nchi ya Korea Kusini kuhusu uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji katika Sekta ya Madini. Dkt. Kiruswa ametoa wito huo wakati akifungua mkutano wa kitaalamu wa African Minerals Geosciences Initiative (AMGI) uliolenga kuonesha maeneo ya kipaumbele sambamba na mkakati wa Serikali kuboresha taarifa za Jiosayansi uliofanyika Agosti 30, 2022 Jijini Dar es salaam. Alisema, mkutano huo umelenga kufunga awamu ya kwanza ya utafiti wa Jiosayansi uliofanyika katika nchi tatu zinazopakana ambazo ni Tanzania, Zambia na Msumbiji kati ya mwaka 2016 – 2021. Dkt. Kiruswa amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania itahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha kwa kuweka mazingira mazuri ya kushirikiana kufanya utafiti zaidi. Aidha, amewaeleza wawekezaji kuwa anatambua nchi ya Korea Kusini ni miongoni mwa nchi zilizoendelea kiteknolojia duniani hatua inayopelekea kuwa na uhitaji mkubwa wa madini ya teknolojia kama vile kinywe, nikeli, niobium na REE. Naye, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini, aliishukuru Serikali ya Korea Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa ya Afrika kwa kuamua kufanya mkutano huo nchini Tanzania na kuahidi kushirikiana katika kuangalia namna ya kufanya tafiti zaidi kwenye maeneo ya nchi. Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania Dkt. Abdulraham Mwanga akizungumza wakati wa kuahirisha mkutano huo wa siku mbili kwa siku ya kwanza, aliwashukuru washiriki wote na kuwakumbusha kuwa madini ni kila kitu kwenye maisha ya sasa hivyo, ni vyema kama Bara la Afrika kukiwa na mkakati madhubuti wa kutambua rasimali madini na kuziendeleza. Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anatarajia kuwasilisha mada namna Benki hiyo inavyoweza kusaidia shughuli za jiosayansi kwa nchi za Afrika. Utafiti wa Jiosayansi ulifanyika katika maeneo ya Tunduma Mkoani Songwe na sehemu ya Wilaya za Tunduru, Namtumbo na Songea katika Mkoa wa Ruvuma chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ya Afrika na kudhaminiwa na Serikali ya Korea Kusini. Mkutano huo umehudhuliwa na washiriki wa mradi wa AMGI kutoka nchi jirani za Zambia na Msumbiji, wawakilishi kutoka GST, wawakilishi kutoka Wizara ya Nyumba, Ardhi na Makazi Nchini Tanzania, Idara ya Upimaji na Ramani, ujumbe kutoka Idara mbalimbali za nchini Korea Kusini ambazo ni Consultancy; Mkurugenzi Msaidizi ofisi ya Kamishina wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi kutoka kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC).

0 Comments:

Post a Comment