Na Peter Mkwavila DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalum mwakilishi wa Wafanyakazi Dk Alice Kaijage amewataka waajiri waendelee kutoa ushirikiano, mazingira rafiki na wezeshi na hamasa kwa watumishi ili washiriki kwenye kuhesabiwa sensa ya watu na makazi.
Dk Kaijage alisema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini Jijini Dodoma kwenye uhamasishaji wa kujiandikisha sensa ya watu na makazi.
Aliwataka waajiri hao kutoa ushirikiano na mazingira rafiki kwa watumishi ili washiriki katika kuandikishwa na kuhesabiwa kwenye sensa hiyo.
Alisema kuwa takwimu sahihi zitawezesha serikali na wadau pia kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali, hivyo basi watumishi wa umma na binafsi wakiwa sehemu ya watanzania wahamasishwe kushiriki kuhesabiwa.
Aidha alisema takwimu sahihi zitakapopatikana zitasaidia kujua idadi ya watu katika maeneo mbalimbali, pia itaweza kuwapatia huduma za kijamii kwa ubora kama vile maji, shule, vituo vya afya, ugani kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kutoa mikopo kwenye makundi.
Hata hivyo, Dk Kaijage ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwa na nia ya dhati ya kuwahudumia watanzania kwa kupanga bajeti kwa kuzingatia takwimu sahihi ya idadi ya watu wake.
“Niipongeze serikali kwa kujipanga kwa kuendesha sensa ya watu na makazi ambayo itakayofanyika Agost 23 mwaka huu, kwa mujibu wa sheria ya takwimu sura 315 ambayo pia ipo kwenye utekelezaji wa mpango mikakati wa umoja wa mataifa wa kufanya sensa unaoanzia 2015-2024”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maaridhiano Mkoa wa Dodoma Askofu Dk Evance Chande aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na dini kushirikiana kwa pamoja na serikali kuelimisha jamii na pale inapotokea upotoshaji wawe tayari kukemea.
Dk Chande alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha watu wake wanaboreshewa maisha yao, hivyo viongozi wa vyama vya siasa na dini waungane kwa pamoja kuelimisha suala hili la sensa ya watu na makazi.
Naye Katibu wa Bakwata mkoa wa Dodoma Husseni Kuzungu ameitaka sensa ya watu na makazi isifananishwe na itikadi yoyote ya imani ya kidini na kwa vyama vya siasa.
Kuzungu alisema kuwa suala hilo la sensa ni la kiserikali na linatakiwa kuheshimiwa na kushiriki kwa vitendo katika kuhakikisha watanzani wote wanajiandikisha kwa lengo la kupata takwimu sahihi kwa ajili ya maendeleo.
Mwisho.
0 Comments:
Post a Comment