Na. Mwandishi wetu Arusha
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema Wizara ya Katiba na
Sheria imekusudia kuhakikisha huduma za kisheria zinazotolewa na Wizara
na Taasisi zilizo chini yake zinapatikana kwa njia ya TEHAMA.
Dkt.
Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa
Wasajili Wasaidizi wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria, Wasaidizi wa
Kisheria, Mawakili, Wanasheria na Maafisa wa Jeshi la Magereza ambayo
inafanyika kuanzia leo Oktoba 17, 2022 Jijini Arusha.
Dkt
Ndumbaro amesema “Kwa kutambua umuhimu wa TEHAMA kwenye utoaji wa
huduma, Wizara ya Katiba na Sheria imekusudia kuhakikisha huduma za
kisheria zinazotolewa na Wizara na Taasisi zilizo chini yake
zinapatikana kwa njia ya TEHAMA. Hili litawezesha huduma kupatikana kwa
wakati na hatimaye kuwezesha vyombo vingine vya utoaji haki kutoa haki
kwa wakati na kwa gharama nafuu.”
Dkt.
Ndumbaro ameongeza kuwa TEHAMA imekuwa na mchango mkubwa kwenye utoaji
wa huduma na utendaji wa Serikali kwa ujumla. Faida zinazopatikana ni
pamoja na kuwepo kwa utunzaji wa kumbukumbu sahihi za wananchi, kuweka
uwazi na uwajibikaji wa utoaji huduma hususan panapokuwa na malalamiko
kutoka kwa wananchi, kurahisisha upatikanaji wa huduma, na vilevile
kuondoa mianya ya rushwa kwenye utoaji huduma kwa kuwa hakuna
mwingiliano kati ya mtoa huduma na mteja.
Dkt.
Ndumbaro alisisitiza kuwa ni vyema kuwa na mifumo mizuri ya kisheria
ambayo itarahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati; mifumo ambayo
itawezesha wananchi kupata huduma za kisheria popote walipo kwa gharama
nafuu katika kuifikia haki. Uwepo wa mifumo, utawapunguzia wananchi muda
na gharama za kushughulikia masuala ya kisheria na badala yake
watajikita zaidi katika shughuli zingine za kiuchumi na kimaendeleo
hivyo basi kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha,
Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa Wizara ina jukumu kubwa la kutoa elimu ya
Katiba na Sheria kwa wananchi hususan vijana kwani hiyo itawasaidia
kujua sheria na kudai haki zao.
Dkt.
Ndumbaro amesema “Naamini kwamba Wizara ina jukumu kubwa la kutoa elimu
ya Katiba kwani huwezi kwenda kutoa kitu kipya wakati hujui cha zamani,
tupate elimu ya Katiba iliyopo sasa ili tujue mazuri yakwenda nayo
katika Katiba mpya na kuacha mabaya yaliyopo.”
Akimkaribisha
Waziri Ndumbaro kufungua warsha hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw.
David Lyamongi amesema Wasaidizi wa kisheria wapewe kipaumbele katika
kutekeleza kazi zao kwani wanasaidia sana jamii hasa wajane na yatima.
Bw.
Lyamongi amesema “mchango wa Wasaidizi wa Kisheria ni mkubwa sana
katika jamii hususan katika Mkoa wa Arusha kwenye masuala ya kisheria
yaliyomshinda mwananchi au kushindwa kwenda mwenyewe mahakamani hivyo
kuhitaji uwakilishi.”
Msajili
wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria nchini Bi. Felistas Mushi amesema
mafunzo hayo yamewashirikisha Watoa Huduma za kisheria kutoka kwenye
Mashirika kumi na tano, Wasajili Wasaidizi na Maafisa Magereza kutoka
mikoa kumi ya Tanzania Bara. Washiriki hao wamechaguliwa kwa sababu wapo
karibu na wananchi sanjali na kuwasaidia wananchi wengi wa chini
waliopo kwenye maeneo yao, alisema Bi. Mushi.
Awali
akitoa maelezo ya utangulizi Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Bw. Gabriel
Ally amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu nne kwa mwaka wa fedha
2022/2023.
Bw. Gabriel
amesema huduma za TEHAMA zinarahisisha kufikisha huduma za kisheria kwa
wananchi popote pale walipo hivyo ni muhimu makundi hayo manne
yakazingatia mafunzo hayo katika utendaji kazi wao kwa kuwa zinahusiana
na wananchi kwa kiasi kikubwa.
Mafunzo
haya yanahusisha mifumo inayohusu usajili wa watoa huduma za msaada wa
kisheria na wasaidizi wa kisheria ambazo zinatolewa chini ya Sheria ya
Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017, mfumo wa usajili wa watoa huduma za
maridhiano, usuluhishi, na upatanishi kama ilivyobainishwa chini ya
Sheria ya Usuluhishi ya Mwaka 2020. Mifumo mingine ni pamoja na
uwasilishaji wa malalamiko, maombi ya huduma za msaada wa kisheria,
maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha mashauri mahakamani nje ya muda
pamoja na huduma nyingine za kisheria.
0 Comments:
Post a Comment