Na mwandishi wetu , Simiyu
MADHARA ya sumukuvu huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi, baada ya muda mrefu kutegemea na kiasi
cha
sumukuvu hiyo iliyopo kwenye chakula kilicholiwa,idadi ya milo ya
chakula kilichochafuliwa na umri pamoja na hali ya afya ya mlaji.
Pia
madhara ya Sumukuvu yanayotokea ndani ya muda mfupi husababishwa na
ulaji wa kiasi kikubwa cha sumukuvu ikiwa ni pamoja na kuathirika kwa
ini, figo, mfumo wa fahamu, uwezo wa damu kuganda na hata kuweza
kusababisha kifo.
Akizungumza
katika maadhimisho ya siku ya chakula duniani yenye Kaulimbiu isemayo
'Uzalishaji bora, Lishe bora, Mazingira bora na Maisha bora kwa wote,
Habaki Mtu Nyuma' ambayo yanafanyika mkoani Simiyu Kaimu Mratibu wa
Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), Khassim Msuya amesema
kuwa Sumukuvu zinapokuwepo kwenye mazao au bidhaa hazionekani kwa macho,
na kwamba huendelea kubaki hata baada ya chakula kupikwa au
kusindikwa.
Ameeleza kuwa madhara husababisha kupungua kwa kinga ya mwili,kushuka kwa uzalishwaji wa maziwa na mayai,upungufu wa damu
,Kukosa hamu ya kula,kuharibika kwa mimba, Kuathiri mfumo wa uzazi, Kuharisha,Kutapika naVifo.
"Mazao
yanayochafuliwa na kuvu ni kama vile nafaka (mahindi, mtama, ulezi,
mchele, ngano, uwele), mbegu za mafuta (alizeti, pamba), karanga,
korosho, jamii ya mizizi iliyokaushwa (mihogo na viazi), viungo
vilivyokaushwa, kahawa, mazao yanayotokana na mifugo (maziwa, mayai),"
alisema Msuya.
Ameongeza
kuwa athari za sumukuvu kiuchumi ni kukataliwa kwa bidhaa za chakula
katika soko la ndani na nje ya nchi,Kuathiri utoshelevu wa
chakula,kuathiri uzalishaji wa mifugo,kuongezeka kwa gharama za
matibabu,kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji mali na kuongezeka kwa
gharama za udhibiti.
"Dalili
zinazoashiria kuwa mazao yamechafuliwa na kuvu wanaozalisha sumukuvu ni
pamoja na ukungu, kuvu, harufu ya uvundo, punje kutengeneza vumbi,
punje kugandamana au punje kubadilika rangi, na kuwa na rangi nyeusi
iliyochanganyika na kijivu, kijani, chungwa au njano," ameeleza Mratibu
huyo.
Amefafanua kuwa
vichochezi vya uchafuzi wa sumukuvu kwenye mazao ya chakula na uwepo wa
mazingira wezeshi kwa kuvu kuota na kuzalisha sumukuvu ni pamoja na hali
ya hewa ,joto-ridi (temperature), unyevunyevu, ukame, mafuriko na mvua
zisizotarajiwa wakati mazao yanapokaribia kukomaa na wakati wa kuvuna.
Amesema
inashauriwa mkulima kutumia mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa au
zile zinazoweza kustahimili hali ya mazingira ya shamba husika.
"
Inashauriwa kutumia mbegu zinazoota na kutoa mazao kwa kipindi kifupi
(mbegu za muda mfupi kulingana na eneo husika) ili kupunguza au kuepuka
muda hatarishi kwa kushambuliwa na kuvu na kuchafuliwa na sumukuvu,"
amesema.
Pia mkulima
anashauriwa kwa kadiri inavyowezekana kubadilisha mazao kwa mzunguko
kati ya yale yanayoathiriwa na yasiyoathiriwa na kuvu,Mfano kupanda
mahindi msimu mmoja na jamii ya mikunde msimu unaofuata
Akizungumzia mafanikio ya TANIPAC, Mratibu huyo amesema hadi sasa
wakulima
61,410 wamepatiwa elimu juu ya udhibiti wa sumukuvu baada ya mavuno
ambapo lengo lilikuwa ni kuwafikia wakulima hao 60,000.
"
Kwa upande wa vijana tumewawezesha vijana 420 kutoka Mamlaka ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wamejengewa uwezo kwenye kutengeneza
Vihenge chuma (Metal silos) ambayo ni mbinu ya kuzuia mazingira wezeshi
ya ukuaji wa kuvu, lengo lilikuwa 400 pamoja na Maafisa ugani 1,351 na
Wanahabari 217,"alisema Msuya.
Mratibu
huyo amefafanua kuwa tulifundisha vijana 420 na sasa tunawafanyia
program atamizi Kwa Kuwafundisha maswala ya ujasiriamali Ili waweze
kutengeneza vihenge kibiashara.
Mratibu
huyo ameeleza kuwa lengo ni kutengeneza vihenge 10,000. Mradi
utapromote vihenge kuhusu hiyo technolojia na kueajulisha wananchi na
kuweza kuwapa fursa ya kutengeneza vihenge hivyo.
CHANGAMOTO ZA MRADI
Mratibu
huyo amesema kuwa Virusi vya Korona (COVID -19), ilizuia mikusanyiko
hivyo mradi ulichelewa kutoa elimu ya ana kwa ana kwa wakulima ambapo
kutumia vyombo vya habari kufikia wakulima hao.
Amefafanua
kuwa mradi huo wa TANIPAC ni wa miaka mitano ambapo ulianza mwaka
2019 na yanatarajiwa kukamilika mwaka 2024, ambao unaotekelezwa
Tanzania Bara na Visiwani – Zanzibar (Unguja na Pemba).
Mratibu
huyo ameongeza kuwa pamoja na changamoto ya COVID -19 lakini wananchi,
taasisi na Wizara tayari wanauelewa wa madhara ya Sumukuvu huku
akitolea mfano Wizara ya Mifugo na uvuvi wameomba kupatiwa elimu ya
sumukuvu.
"Watu wanaokuja
kwenye banda letu katika maadhimisho haya tayari wana uelewa wa
Sumukuvu ila wanataka kujua baadhi ya vipengele wanavyokabiliana navyo,"
amesema Msuya.
Siku ya Chakula Duniani huadhimishwa Oktoba 16, kila mwaka katika nchi zipatazo 150 ikiwamo Tanzania.
Lengo
la maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu Usalama wa Chakula,
utambuzi na usimamizi wa athari zitokanazo na chakula pamoja na
kuboresha afya za binadamu kupitia utoaji wa elimu hiyo.
Shirika
la Chakula na Kilimo na Umaja wa Mataifa (FAO), na serikali ya Tanzania
kupitia program inayo na Umoja wa Ulaya Agree Connect imegundua kampeni
ya kitaifa ya 'Lishe Bora ni Mtaji' ili kujenga tabia ya zinazofaa za
milo hapa nchini kwa kutumia vyakuka vinavuopatikana Tanzania.
Kaimu Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania
(TANIPAC), Khassim Musya akitoa elimu wa wananchi waliofika katika
maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yenye Kaulimbiu isemayo
'Uzalishaji bora, Lishe bora, Mazingira bora na Maisha bora kwa wote,
Habaki Mtu Nyuma'
ambayo yanafanyika mkoani Simiyu.
0 Comments:
Post a Comment