Subscribe Us

SERIKALI INAENDELEA KUWEKEZA KWA WATAALAMU WA NDANI WA MIFUMO

Na WAF - DSM

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza kwa Wataalamu wa ndani wa mifumo ili kuhakikisha miradi yote inayoanzishwa na Wafadhili inaendelea kusimama siku Wafadhili wanapomaliza muda wao. 

Dkt. Shekalaghe ameeleza hayo, katika majadiliano ya pamoja yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya na OR TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la PATH linalotekeleza mradi wa "matumizi ya sahihi ya takwimu" (Data Use Patnership - DUP) yaliyofanyika usiku wa Oktoba 12, 2022 Jijini Dar es Salaam. 

Amesema, Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya mifumo katika maeneo mbalimbali, hususan katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wananchi kwani inasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji na itasaidia kupata takwimu sahihi na kwa wakati ambazo zitasaidia katika kupanga matumizi sahihi na udhibiti wa magonjwa. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anaeshughulika na masuala ya Afya OR TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesema, ili nchi ipige hatua kwa kasi ni muhimu mifumo ipewe kipaumbele kwani inasaidia kufanya ufuatiliaji na kuongeza utendaji katika maeneo ya kazi na kuepuka gharama zisizo za lazima. 

Aidha, Dkt. Magembe amesema, licha ya kazi kubwa kufanyika katika kuboresha mifumo nchini bado ipo haja ya kuongeza kasi ya uwekezaji katika eneo hilo ili mifumo iweze kuwasiliana baina ya mfumo wa hospitali moja kwenda hospitali nyingine (interoperability), jambo litalosaidia kupunguza gharama kwa mwananchi kwa kuepuka kurudia kufanya vipimo.

Aliendelea kusisitiza kuwa, ni muhimu Wadau kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya nchini kupitia matumizi ya mifumo ili kupunguza matumizi ya taarifa za makaratasi, hali inayohatarisha usalama wa taarifa hizo na takwimu katika maeneo ya kutolea huduma. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa Data Use Patnership (DUP) Dkt. Seif Rashid amesema, matumizi sahihi ya takwimu yanasaidia kufanya maamuzi sahihi, hususan katika kutenga fedha na rasilimali watu kwa usahihi na kwa wakati kulingana na mahitaji. 

Nae, Mkurugenzi wa Tehama OR-TAMISEMI Bw. Eric Kitali amewataka Mashirika na Taasisi kutoka nchini kupenda kuwatumia Wataalamu wa ndani kutengeneza mifumo yao ili kutunza taarifa za taasisi zao, pia kufanya hivyo ni ishara ya uzalendo.

"Tupende vya nyumbani, tupende mifumo inayotengenezwa na Wataalamu kutoka ndani ya nchi, pia itasaidia kuongeza usalama."Amesema. 

Mwisho.
 
 
 

 
 

 

 

0 Comments:

Post a Comment