Subscribe Us

*”WANANCHI CHANGAMKIENI MBOLEA YA RUZUKU” RC DODOMA*

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati ametembelea kiwanda cha mbolea cha Intracom Tanzania 
, kiwanda kinachozalisha mbolea kilichopo eneo la Nala Jijini Dodoma.

Mhe. Senyamule ametembelea kiwanda hicho akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na baadhi ya wataalam wa idara mbalimbali.

Mhe. Senyamule ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya zoezi la usajili kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku kwani zoezi bado linaendelea
“Wananchi endeleeni na usajili kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku kutoka Serikalini kwani Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo hasa kupitia kiwanda hiki, tutapata mbolea ya kutosha kwa kilimo bora” .

Akizungumzia uwekezaji wa viwanda katika Mkoa wa Dodoma, RC Senyamule amesema;
“Nawapongeza sana Kiwanda cha Intracom kwa kuwa wa kwanza kuwekeza katika eneo hili la Nala kwani hili ni eneo limetengwa maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na nyinyi hamukuhofia kuwa wa kwanza kuwekeza hapa licha ya changamoto kadhaa, mumeona muwe njia kwa wengine. Natoa wito kwa wawekezaji wengine wote waliochukua maeneo hapa eneo la Viwanda Nala kuja kuwekeza kwani tunatamani tuanze kuiona dhamira hasa ya eneo hili na Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha wawekezaji wanakaa katika mazingira mazuri hapa Dodoma kwani Dodoma ni Fahari ya Watanzania”. Amesisitiza Senyamule.

Kadhalika, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Nduwimana Wazaire, akielezea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda mpaka sasa, amesema kuwa ujenzi unafanyika kwa awamu na kwa sasa tayari awamu ya kwanza imekamilika yenye uwezo wa kuzalisha mbolea tani laki mbili na wanatarajia kuanza ujenzi wa awamu ya pili mwishoni mwa Oktoba . Ujenzi kamili wa awamu ya tatu ambayo ndiyo itakua ya mwisho unatarajiwa kukamilika mwaka 2023.

Kiwanda cha Intracom Tanzania Ltd. kilianza ujenzi wake mapema mwaka jana na kinatarajiwa kuzalisha mbolea kiasi cha tani laki sita kwa mwaka. Kiwanda hiki  kinazalisha aina tatu za mbolea ambazo ni mbolea ya kuoteshea mazao (Fomi otesha), mbolea ya kukuzia (Fomi kuzia) pamoja na mbolea ya kunenepesha mazao (Fomi nenepesha). 

Aina zote hizi tatu zinapotumiwa na mkulima zitasaidia kupata matokeo chanya kwenye kilimo na mbolea inayozalishwa na kiwanda hiki ni (Organo-minerals) yaani mchanganyiko wa samadi na madawa.

MWISHO
 
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati ametembelea kiwanda cha mbolea cha Intracom Tanzania

 

 kiwanda kinachozalisha mbolea kilichopo eneo la Nala Jijini Dodoma

 

0 Comments:

Post a Comment