Subscribe Us

WAZIRI WA SHERIA DKT DAMAS NDUMBARO AMETOA UFAFANUZI KUHUSU WANAFUNZI WA SHERIA KUFELI MAFUNZO KWA VITENDO

Na. Kadala Komba Dodoma 
 
 
 
Kumekuwa na sintofahamu  kuhusiana na matokeo ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), mjadala ulioibuka katika sehemu  mbalimbali kwamba kwa nini wanafunzi hao wanafeli sana. Mjadala huu sio mpya, ni wa muda mrefu.

Historia ya wanafunzi  wachache kufaulu mitihani ya Taasisi hii haijaanza leo, ni ya siku nyingi, lakini hailengi kumkomesha mtu yoyote bali inalenga kuweka viwango vya juu.

Waziri wa katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amezungumza haya katika kikao na waandishi wa habari jijini Dodoma alisema Vinawekwa viwango vya juu kwa sababu Sheria ni jambo muhimu katika utawala bora, utawala wa Sheria, kuleta amani na utulivu pamoja na utoaji wa haki, hivyo ni lazima tuwe na imani na wanasheria tunaowapa jukumu hilo,
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ina Walimu 95 ambapo Walimu 14 kati yao waliobobea katika maeneo mbalimbali ya Sheria wameajiriwa  ajira ya kudumu. 

Kwa uhalisia wa kazi hii hufanyika kwa vitendo, Walimu wengi  wanaochukuliwa ni wataalam waliobobea kwenye maeneo yao ambapo kati ya Walimu 81, Walimu 10 ni Majaji. Kati ya Majaji kumi, watatu ni Majaji ambao bado wako kazini na Majaji saba ni wastaafu ambao wana uzoefu wa kutosha.

Katika orodha ya Walimu 81, Walimu wanne ni Mawakili wa Serikali ambao wengi wamekaa muda mrefu katika nafasi zao na wana uzoefu wa kutosha na Walimu 56 ni Mawakili wa kujitegemea waliobobea katika kazi zao.

 Tangu Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania imeanzishwa, wanafunzi 8,255 kati ya wanafunzi 13,974 wamefaulu sawa na asilimia 59.074 na wanafunzi waliofeli baadhi ya masomo ambao wanaruhusiwa kurudia masomo hayo ni asilimia 21.619.

Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia kubwa ya wanaorudia baadhi ya masomo waliyofeli huwa wanafaulu, hivyo ufaulu kwa ujumla utakuwa kwenye asilimia 81.

Kwa takwimu hizi za ufaulu, asilimia ya waliofeli kabisa ni asilimia 19 kati ya asilimia 100 ambayo ni asilimia ndogo na inatokea kokote duniani.

Kama kuna mwanafunzi anayehisi ameonewa, kuna mfumo wa kukata rufaa ambao upo na unafanya kazi.

Serikali imeunda Kamati ya watu saba ambayo imepewa siku 30 kuleta taarifa juu ya tuhuma hizi.  Kamati hii haijahusisha Waalimu wala Mstaafu yeyote wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) wala Walimu kutoka Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria, tumehusisha wadau wengine ili walete majibu ya ukweli na yenye tija.
 

 

WAKATI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA, DKT. DAMAS NDUMBARO AKITOA UFAFANUZI MBELE YA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DODOMA KUHUSU WANAFUNZI WA SHERIA KUFELI MAFUNZO KWA VITENDO*



 

0 Comments:

Post a Comment