Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amekemea Vikali kuhusu upotoshaji mbalimbali unaosambaa kwenye mtandao ya kijamii kuhusu Jeshi la kujenga Taifa na kuwahakikishia Watanzania kuwa JKT ni mahali sahihi na muhimu kwa vijana kuongeza tija katika Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 13,2023 wakati akifunga mafunzo ya 19 kwa mujibu wa Sheria Operesheni ya miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa, katika viwanja vya 834 KJ Makutupora Jijini Dodoma.
Amesema lengo kuu la vijana kuhudhuria mafunzo hayo ya mujibu wa Sheria ni kuwajengea Uzalendo, Moyo wa Kupenda kazi, kuwapa mbinu za kujitegemea, kujenga umoja na mshikamano utakao imarisha umoja wa kitaifa ili kuwa na Taifa bora lenye ustawi mzuri na viongozi bora wenye fikra chanya kwa Taifa .
"Nimefurahishwa na tamko lenu mlilolitoa leo juu ya upotoshaji mbalimbali juu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Nami nawahakikishia Watanzania JKT ni mahali sahihi na muhimu kwa vijana wetu ili kuongeza tija ya utaifa wetu, hivyo mtoto akipata nafasi ya kujiunga na JKT ni fursa nzuri na aitumie" amesisita Senyamule
Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule amewaasa vijana wahitimu hao kuwa na matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa kupata elimu na kufanya biashara za njia ya mtandao.
"Napenda kuwasihi sana mkaitumie mitandao kwa ajili ya kujielimisha na siyo kutumia kuangalia mambo yasiyofaa ambayo ni kinyume na maadili yetu hivyo kuchangia mmomonyoko wa maadili
"Amesisitiza Senyamule
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo ametumia jukwaa hilo kuwaasa wananchi wanaochoma moto ovyo katika eneo la Kikosi ambalo pia ni eneo oevu la bonde la Mzakwe ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji kwa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanatunza mazingira yake.
"Wananchi tunaoishi maeneo ya kuzunguka bonde tafadhali sana tutunze maeneo haya ili tuweze kuwa na uhakika wa maji kwani maji ni Uhai, yeyote atakaye kutwa anafanya shughuli ambazo zinachangia kuharibu mazingira kama uchomaji mkaa, kukata miti na Kilimo atachukuliwa hatua za sheria "amehimiza Senyamule
Kwa Upande Wake, Kaimu Kamanda Kikosi Meja James Andrew Macheta amesema wahitimu hao wamefanikiwa kujifunza Ukakamavu, Utii, Ujasiri, Stadi za Maisha, Ujasiriamali pamoja na ulinzi wa Taifa sambamba na kufanya kazi bila kuchoka sehemu yeyote hivyo wako tayari kutumika kama walinzi sehemu yeyote watakapo hitajika .
Vilevile, amewahasa vijana hao kuwa mabalozi wazuri kwa yote waliyojifunza kwa muda wa miezi mitatu kwa kuwa Wachapakazi na Kutekeleza kwa vitendo yote waliyofunzwa .
Home »
» JKT NI MAHALI SAHIHI NA MUHIMU KWA VIJANA-MHE SENYAMULE
0 Comments:
Post a Comment