Na WAF, Dodoma.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Afya inatarajia kuendesha Kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya Milioni 3,250,598 walio chini ya miaka 8 kwenye Mkoa wa Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Jijini Dodoma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio ambayo inatarajiwa kuanza kufanyika nchini kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2023.
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania inaendesha Kampeni hiyo ya chanjo kutokana na Wizara kupokea taarifa mnamo Mei 26, 2023 za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili za kupooza kwa ghafla.
Mtoto huyo ambaye alitolewa taarifa kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Uchunguzi wa Maabara ulithibitisha kuwa mtoto huyu ana maambukizi ya virusi cha Polio.
Waziri Ummy amesema kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia hivyo hali hii inaongeza tishio na hatari ya maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo.
“Napenda nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane (8). Kampeni hii itafanyika kwa siku nne (4) kuanzia tarehe 21 – 24 Septemba, 2023 katika Mikoa sita (6) inayopakana na nchi zenye mlipuko wa Polio ambayo ni Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya”. Amesema Waziri Ummy.
“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili (Polio Virus Type 2) kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu. Kwa Mkoa wa Rukwa tunatarajia kufikia watoto 391,883 Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe 402,643”. Amefafanua Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Ili kufanikisha Kampeni hii, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Wadau wa chanjo imeshafanya maandalizi kwa ajili ya kuwezesha zoezi bila kuathiri shughuli zingine za wananchi.
“Wakati wa Kampeni kutakuwa na jumla ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa yote sita (6) itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu. Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo Nyumba za Ibada”. ameeleza Waziri Ummy na kutoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo dhidi ya Polio, imeundwa timu ya watu waliopata mafunzo ya kutoa chanjo hiyo katika Mikoa hiyo sita.
“Tumeunda timu nzuri ambayo imepata mafunzo ya kutoa chanjo ambayo ina watoa huduma Elfu Tano Mia Mbili Tisini na Moja (5,291) katika Mikoa hiyo Sita ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa katika kupatiwa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio” amesema Prof. Nagu.
“Tunawapa hamasa wazazi wahakikishe kwamba, wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto wetu kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia chanjo”. Ameongezea Prof. Nagu.
Home »
» WATOTO ZAIDI YA MILIONI 3 KUPATA CHANJO YA POLIO KWENYE MIKOA 6 NCHINI.
0 Comments:
Post a Comment