Subscribe Us

CHUO KIKUU CHA UDOM KUSHIRIKIANA NA CHUO KIKUU CHA COLONY

Na Sifa Lubasi, Dodoma



CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Colony kilichopo Ujerumani kimefanya warsha ya watafiti wa kuhifadhi maarifa asilia kwa kuwashirikisha wataalam kutoka nchi tisa duniani kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika uhifadhi kumbukumbu Kwa vizazi vijavyo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Lughano Kusiluka akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu warsha hiyo alisema kuwa warsha hiyo ina matarajio makubwa katika kusaidia kuhifadhi maarifa asilia ambayo kwa namna moja au nyingine yameanza kusahaulika.

Alisemakuwa hilo  kutokana na jamii kujikita zaidi Katika elimu ya magharibi.





Alisema kuwa moja ya mikakati ya kufanikisha hilo kuwa ni pamoja na kufanya utafiti na kukusanya maarifa ya asili ya Kiafrika kutoka kwa wazee  na jamii za asili na hiyo itasaidia kuhifadhi maarifa na desturi ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu.



Alisema kuwa jamii inatakiwa kuweka kumbukumbu za mila na desturi za Kiafrika kwa njia ya hadithi, nyimbo, na ngonjera,kumbukumbu hizo zitatusaidia kuelewa na kuheshimu urithi na kujifunza  kuelewa kalenda za Kiafrika na matukio ya kihistoria yaliyotokea katika bara la Afrika.

“Watanzania tunatakiwa kujua kuwa tunaishi katika bara tajiri lenye historia ndefu, na ni muhimu kuelimisha na kuenzi historia hii,” alisema



Profesa Kusiluka akielezea kuhusu maono ya UDOM kwa miaka ijayo alisema kuwa Chuo hicho kinatarajia kulitumia Jengo la Chimwaga kama hifadhi ya lugha asili za Tanzania na tamaduni mbalimbali jambo litakalo wavutia wengi na kuwa kivutio cha utalii.



"Kupitia uhifadhi huu tunategemea kuwashirikisha vijana wetu katika shughuli za kijamii ambazo zinahusisha tamaduni na urithi wa Kiafrika na Kuwafundisha na kuwahusisha vijana wetu kutahakikisha kuwa maarifa haya hayapotei,"amesisitiza Prof.Kusiluka.



Naye mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Colony, Getrude Shnerider alisema kuwa warsha hiyo inaangazia pia namna ya uhifadhi wa viumbe hai na wanyama

lengo ni kusaidia jamii kutenga maeneo ya asili kama vile misitu, mabonde na maeneo mengine ambayo ni muhimu kwa tamaduni na urithi .



Mmoja wa washiriki katika warsha hiyo ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu(PhD)Adriano Utenga alisema kuwa maarifa ya watu yanatunzwa na watu wenyewe hivyo kutoa wito kwa watanzania kuungana na nchi nyingine za Kiafrika kwa njia ya ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa ili kudumisha umoja  na kulinda tamaduni.

Akitoa mfano alisema nchi za Ghana na Senegal zimefanya jitihada kubwa za kuhifadhi tamaduni na urithi zao.



Mwisho



 



0 Comments:

Post a Comment