Subscribe Us

JUKUMU LA KUWAANGALIA WAZEE SIO LA SERIKALI PEKEE.

Na Moreen Rojas Dodoma



Katika nchi nyingi Duniani,Wazee wamekuwa wakituzwa isipokuwa kwamba kila nchi ina namna yake ya kuwatunza wazee wao kwa kulingana na mila,desturi na tamaduni pamoja na hali za kiuchumi za nchi zao.

Hayo yamesemwa na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein wakati wa mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya uzee uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Shein amesema kuwa kwa hapa nchini Tanzania suala la kuwaenzi na kuwatunza wazee ni utamaduni wa kale uliotokana na mila na desturi zetu.

Miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanyika ni kuwajengea wazee hao nyumba imara za kuishi za ghorofa zilizokuwa na vifaa mbalimbali vya umeme vya kutumia,wazee hao waliwekwa pamoja na kuyaendeleza maisha yao vizuri.

Nyumba hizo za wazee zimejengwa huko Sebleni katika wilaya ya Mjini na Welezo katika Wilaya ya wete.

Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba nyumba hizo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo kila haja ya kufanya hivyo inapotokea na hadi leo zinaendelea kutumiwa na wazee.

Kadhalika wazee waliopatiwa makaazi katika nyumba hizo wanaendelea kuhudumiwa na Serikali katika mahitaji yao yote ya msingi.

Mbali na jitihada hizi, matamko ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutangaza elimu bure kwa wote tarehe 23 Septemba,1964 na matibabu bure kwa wote tarehe 23 Machi,1965 yalisaidia sana katika kuwaendeleza wazee na kuwawezesha kukabiliana na uzee na maradhi.

Aidha ameongeza kuwa katika kuendeleza falsafa za waasisi wetu wa taifa la Tanzania,taifa letu limekuwa likichukua hatua zaidi kusaidia hali za wazee kwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Katika miaka kadhaa iliyopita TanzaniaBara,Mpango wa TASAF II uliweka kima cha shilingi za Kitanzania 6000 kila mwezi kuwasaidia watu wenye mazingira magumu wakiwemo wazee.

Kadhalika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya Mpango wa Pensheni Jamii,ilianzisha utaratibu wa kuwasaidia wazee kwa kima cha Tsh.5,000 kila mwezi.

Kima hiki cha fedha hakikuwa kikikidhi mahitaji kwa wazee walioko TanzaniaBara na hata kwa wale wa Zanzibar,lakini hatua hiyo ilikuwa ni muhimu sana kama mwanzo wa kuelekea katika uundaji wa Sera na Sheria Madhubuti za hifadhi ya jamii kwa wote.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa idadi ya wazee ni asilimia 4.5 watu wote hapa nchini,hata hivyo matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika hivi karibuni yatatupa idadi halisi ya wazee tulionao kwa sasa,ili tuweze kutumia vizuri takwimu hizo katika kuweka mipango mizuri ya kuwaletea maendeleo.

Kauli mbiu ya mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya uzee ni "Miaka 60 ya Uhuru,Tuko wapi na tunakwenda wapi?
 
 

 

 

0 Comments:

Post a Comment