Home »
» *YALIYOJIRI SEPTEMBA 1, 2022 JIJINI DODOMA WAKATI SERIKALI IKITOA UFAFANUZI KUHUSU TOZO*
*YALIYOJIRI SEPTEMBA 1, 2022 JIJINI DODOMA WAKATI SERIKALI IKITOA UFAFANUZI KUHUSU TOZO*
*Aliyosema Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba*
#Chimbuko la tozo lilikuwa ni kwa ajili ya kuunganisha nguvu kama Watanzania ili tuweze kutekeleza baadhi ya mahitaji ya lazima ambayo yamekuwa yakikosa bajeti kutokana na bajeti zinazopangwa.
#Katika nchi za Afrika Mashariki na SADC, hakuna nchi inayotekeleza kwa mara moja miradi mikubwa kama Tanzania, hii inapelekea uhitaji wa bajeti yetu kuongezeka kwa sababu ya miradi mikubwa inayotekelezwa.
#Katika mwaka 2021, kati ya tozo zilizokusanywa, Shilingi bilioni 221 zilienda kwenye mikopo ya elimu ya juu, Shilingi bilioni 117 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na fedha zingine zilienda kwenye ujenzi wa madarasa.
#Tozo hii sio kodi ya biashara wala haitokani na faida ya biashara bali chimbuko lake ni ushirikiano wa pamoja, ilivyokuwa inafanyika mwanzo ilitamkwa kama kodi ya miamala ya simu, kwa sababu tunataka kushirikisha watu wengi tuliona tuwashirikishe hata wanaofanya miamala ya kibenki.
#Tumeendelea na tozo mwaka huu kwa sababu mbali na madarasa na vituo vya afya, kuna mambo mengine ya msingi yenye umuhimu wa kuchukuliwa hatua kwa haraka ikiwemo shughuli za uzalishaji ili zisaidie watanzania wapate ajira.
#Kuanzia sasa mpaka mwezi Januari, 2023 kupitia tozo, tumepanga kujenga madarasa yasiyopungua 8,000, kumalizia vyuo vya VETA katika wilaya 72 zilizobakia pamoja na vitendea kazi katika vituo vya afya.
#Tumesikia maoni ya wananchi na tumeyapokea na tumekutana na wataalam na makundi mbalimbali, ikiwemo kutozwa tozo mara mbili pale unapotoa benki kwenda kwenye simu na ukiituma kwenye simu kwenda kwa mtu mwingine, tumepokea na tunafanyia kazi. Tutatoa majibu ya utekelezaji wake hivi karibuni.
#Maoni mengine ni kuhusu tozo iliyokusanywa kutoka kwenye mabenki ambayo ilitakiwa kuanza tarehe 1, Serikali imejiridhisha kwamba kuna baadhi ya taasisi za fedha zimeanza kukusanywa tarehe tarehe 15 lakini zimekata fedha kuanzia tarehe moja. Tumeona mantiki kwenye jambo hili nalo tutalifanyia kazi.
#Kodi ya upangishaji majengo sio Sheria mpya isipokuwa utekelezaji wake ndio umeanza wakati huu, anayepaswa kulipa kodi ya kupangisha ni mwenye nyumba. Kuhusu mpangaji kukusanya kodi hiyo badala ya TRA wenyewe. Serikali imepokea maoni hayo na inafanyiwa kazi.
#Watu wanaostahili kulipa kodi na hawalipi, wanasababisha wengine wanaolipa kodi kubeba mzigo mkubwa ndio maana kodi zetu zinakuwa juu.
#Tumeweka timu zinaendelea kuchambua kuhusu mifumo yetu ya kodi, mtu ambaye ana mapato ni lazima alipe kodi iliyo sahihi.
*Aliyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa*
#Hadi kufikia Disemba, 2020, Serikali imejenga Hospitali za Wilaya 102, Vituo vya Afya 487, Zahanati 1,198, kwa kipindi cha mwaka na miezi mitano ambao Rais Samia amekuwa madarakani, katika Tarafa 570 tumeshajenga Vituo vya Afya kwenye tarafa 207. Kupitia tozo za miamala ya simu, tumejenga vituo vya afya 234 kwa Shilingi bilioni 117.
#Serikali imetuwezesha Shilingi bilioni 149.5 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa tiba vya kisasa kwenye vituo hivyo vilivyojengwa kupitia fedha za tozo.
#Tusingeweza kufikia katika hatua hii kwenye sekta ya afya kama zisingekuwa tozo hizi, nawahakikishia kuwa tutaendelea kusimamia vyema makusanyo tutakayoendelea kuyapata kupitia tozo hizi ili kuhakikisha huduma katika sekta ya afya zinaendelea kuwa bora.
*Aliyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu*
#Nawahakikishia wafanyakazi kuwa kuhusu maoni yao yanayohusu tozo, wasiwe na mashaka na uwakilishi wa vyama vyao vya wafanyakazi kwenye suala hilo.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*
0 Comments:
Post a Comment