Imeelezwa
kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais
Mhe. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Madhehebu ya dini kupitia
mahubiri na kufundisha neno la Mungu kwa watu wote.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko katika Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 75 ya Kanisa la Elimu Pentekoste Tanzania (KEPT)
iliyofanyika Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Akizungumza
kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Dkt. Biteko
ametoa pongezi kwa niaba ya Serikali kwa mambo yanayofanyika ya kuhuburi
kwa watu na Taifa kwa ujumla ikiwemo kufundisha neno la Mungu kwa watu
wote.
Pia, amewapongeza
kwa kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya, kuendelea kuhimiza
waumini wote kudumisha amani, upendo, mshikamano na utulivu kwa kufanya
kazi kwa bidii pamoja na kutunza mazingira.
Dkt.Biteko
amesema, Mhe. Rais Samia ameendelea kusisitiza kuwahudumia watanzania
kwa heshima kubwa ili maisha yao yazidi kuwa bora kila wakati.
"Nitoe
mfano kwa sekta ninayoiongoza ya Madini, tangu Mhe.Rais ameingia
madarakani ametuelekeza kufuta baadhi ya kodi mbalimbali ambazo
wachimbaji wadogo walikuwa wanaona ni kero katika shughuli zao.
Pia,
Mhe. Rais amesisitiza kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wa
ndani na nje kwa kufuta baadhi ya vipengele vya Sheria na Kanuni ambavyo
vilikuwa vinakwaza uwekezaji.
"Yote
haya, Mhe. Rais anayafanya kwa sababu kiu yake ya kuona kila mwananchi
ndani ya nchi hii anakuwa na furaha na maisha yake, na kufurahia kufanya
kazi anayoifanya kwa ajili ya kuendeshea maisha yake," amesisitiza Dkt.
Biteko.
Aidha, Dkt.
Biteko kwa niaba ya Makamu wa Rais ameshiriki katika uwekaji wa jiwe la
msingi wa ujenzi wa jengo la kanisa na upandaji wa mti wa kumbukumbu.
Kwa
upande wake, Baba Askofu Mkuu wa KEPT, Peter Konki amesema, kanisa
lilianzishwa na Wamisionari kutoka Uingereza mwaka 1946 nchini Tanzania.
Amesema,
walifungua makanisa ya kwanza wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma, Msolwa
katika mkoa wa Pwani, Tanga na wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Askofu
Konki ametoa wito kwa jamii na watanzania kushiriki katika kudumisha
amani na utulivu iliyopo kwa vitendo na kuendelea kufanya kazi kwa bidii
na kuishi maisha mema.
Hafla
ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 ya KEPT imehudhuriwa na Naibu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Babati, Pauline Gekul, Maaskofu Wakuu kutoka Madhehebu mengine na
waumini mbalimbali.
0 Comments:
Post a Comment