Na Moreen Rojas,
Dodoma.
Wiki ya huduma za fedha inalenga kuwafikia wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma,wanafunzi,wakufunzi,wanawake,vijana,watu wenye mahitaji maalumu,wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs),waendesha boda boda,machinga,asasi za kiraia,wahariri na waandishi wa vyombo vya habari,watoa huduma za fedha,watoto na umma kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na kamishna wa maendeleo ya sekta ya fedha kutoka wizara ya fedha Dk.Charles Mwamwaja wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa wizara hiyo jijini Dodoma kuelezea maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa tarehe 20 hadi 26 novemba 2023 katika uwanja wa sheikh Amri Abeid Arusha.
Aidha ameongeza kuwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi watashiriki na wanaendelea kualikwa kushiriki katika maadhimisho haya ikiwa ni pamoja na Wizara,idara na wakala wa serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
"Wasimamizi wa Sekta ya fedha,taasisi za fedha,asasi zisizo za kiserikali,sekta binafsi,bodi za wataalamu,vyama vya wafanyakazi,vyombo vya habari,taasisi za elimu na utafiti,washirika wa maendeleo,vyama vilevile vya sekta ya fedha,makundi ya watoaji wa huduma za fedha na taasisi za dini zinazotoa huduma hizo" Ameongeza Dk.Mwamwaja.
Aidha amesema njia mbalimbali zitakazotumika katika kutoa elimu ya fedha kwa umma ikiwemo,machapisho(vipeperushi na mabango madogo),uandishi wa insha,gari la matangazo,semina,maonesho ya bidhaa za fedha,majukwaa ya kidigitali(mfano,simu za kiganjani),mitandao ya kijamii,vyombo mbalimbali vya habari(Tv,Radio,Magazeti)pamoja na burudani.
"Malengo ya wiki ya huduma za fedha ni kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini,kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia elimu ya fedha,kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha,kutoa elimu ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha,kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha,kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao,kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba,kukopa na kulipa madeni na kuongeza kwa mchango kwa mchango wa sekta ya fedha kwenye ukuaji wa uchumi" Amesisitiza Dk.Mwamwaja.
Sanjari na hayo utekelezaji wa wiki ya huduma za fedha unatarajiwa kuwa na matokeo chanya kwa mtu binafsi,kaya,jamii na taifa kwa ujumla kwa kuongezeka kwa idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu wa elimu ya fedha na maarifa juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za kifedha,kuimarika kwa uelewa na matumizi ya masoko ya fedha,kusogeza huduma za fedha karibu zaidi na wananchi,kuimarisha matumizi ya huduma hizo pamoja na kupata maoni na ushauri wa kuboresha huduma hizo,kuwawezesha watumiaji wa huduma za fedha kuelewa haki na wajibu wao,kuwawezesha wananchi kupata maarifa kuhusu namna bora ya kusimamia vizuri rasiliamali fedha,kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao,wananchi kupata maarifa na uelewa wa masuala ya fedha na hivyo kuwezesha kujenga utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Kauli mbiu itakayotumika katika wiki ya huduma za fedha kitaifa ni "ELIMU YA FEDHA,MSINGI WA MAENDELEO YA KIUCHUMI".
Home »
» WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA INALENGA KUWAFIKIA WADAU MBALIMBALI.
0 Comments:
Post a Comment