Subscribe Us

WAHALIFU WOTE MKONO WA SHERIA UTAWAANDAMA" NAIBU WAZIRI SAGINI

 
Na Mwandishi WNN,

Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini amewataka Wananchi wa Mkoa wa Mara Wilaya ya Butiama kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kutoa taarifa za siri kwa wale wote wanaoshiriki katika matukio mbalimbali ya  kihalifu  ili waweze kubainika, kuchukuliwa hatua za Kisheria na  Wananchi waweze kuondokana na hofu na  kuendelea na shughuli zao za  kiuchumi kwa Amani na Utulivu.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo jana tarehe 31 Mei, 2023 wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mmazami Kata ya Bukabwa na Wananchi wa Kijiji cha Mwibagi Kata ya Kyanyari Wilayani Butiama kufuatia kuripotiwa kwa vitendo vya kihalifu vilivyoanza kushamiri  katika siku za karibuni katika Wilaya ya Butiama yakiwemo mauaji, kujeruhiwa kwa vijana 8 wanaoshiriki katika  ulinzi shirikishi na matukio ya wizi.

“Serikali imesikitishwa sana na matukio ya takribani wiki mbili yaliyotokea katika Wilaya ya Butiama. Ninawapa pole sana kwa niaba ya Serikali kwa wote mliokumbwa na changamoto hiyo. Faraja yangu ni kwamba kwa Wananchi wote mliozungumza hapa hakuna aliyetayari kuona Wananchi ambao wamejitahidi kujitafutia mali zao wanakuja kudhuriwa na watu ambao ni wavivu, hawajiangaishi na kufikiri wanaweza kujinyanyua kiuchumi kwa kupora mali za wenzao hilo halikubaliki kwa vyovyote vile. IGP Wambura amefanya mabadiliko ya Viongozi wa Kipolisi katika Mkoa wa Mara na ameleta Makamishna wawili kutoka Polisi Makao makuu. Hawa wote walioletewa katika Mkoa wa Mara wapo kazini naomba muamini kwamba Wahalifu wote waliofanya uhalifu huu Mmazami na Vitongoji vyake watapatikana na mkono wa Sheria utawaandama. ”Alisema Naibu Waziri Sagini

Aliendelea kusema “Wahalifu hawa wanatoka katika Familia zetu. Watakapokuwa wanashughulikiwa tunaomba hata kama wewe ni mzazi wake mtuunge mkono. Nataka niwaambie mtu anaanza kujifunza kuiba akiwa nyumbani mnaponyamaza na kuwatetea hasa Wakinamama mnafanya makosa. Madhara yake akizoea uhalifu anakwenda kuiba kwa mwingine”Alisema Naibu Waziri Sagini

Kamishna wa  Operesheni na  Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi CP Awadhi Haji  amesema kuwa kwa matukio yote  yaliokwisha kutokea hatua kali zimeanza kuchukuliwa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya usalama ikiwa ni pamoja na kuwabaini baadhi ya Wahalifu katika matukio mbalimbali na  amesema kuwa  wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine watakamatwa ili kukomesha na kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyofanyika na kuepuka kujirudia tena.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama na Mwenyekiti wa Kamati ya  Ulinzi na Usalama  Wilaya Mwalimu Moses Kaegele amesema kuwa upo utaratibu wa kuwa na “YOWE” kwa  maana ya ulinzi shirikishi Lakini utaratibu huo umekuwa ukifanyika kwa kutozana faini jambo ambalo amelipiga marufuku kwani faini hizo hazipo kwa mujibu wa sheria na miongozo. Kaegele amesema kuwa utaratibu wa ulinzi shirikishi wa  “YOWE” ni muhimu sana na ni lazima  na ameelekeza Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kutoa elimu kwa jamii juu ya namna bora ya kutekeleza hilo kwa kuwa na mahusiano kati  ya Serikali ya Kijiji, Polisi na watu wa “YOWE” wakati taratibu nyingine za kuwepo kwa sheria za faini zikiendelea kwa mujibu wa uandaaji wa  sheria ndogo zinazosiamamia ulinzi  na Usalama katika uendeshaji wa Serikali za  Mitaa.

Awali wakizungumza kwa namna tofauti na kuonesha hali ya masikitiko kufuatiwa uwepo wa vitendo hivyo vya kihalifu baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Butiama wakiwemo Matiku Masero, Joshua Warioba na Edwin Ole  wamesema kuwa zipo sababu mbalimbali zinazopelekea uwepo wa matukio hayo ikiwa ni baadhi ya Wahalifu licha ya kukamatwa lakini bado baada ya muda huwa wanaachiliwa jambo ambalo linakatisha tamaa Wananchi na pia kuleta ongezeko la visasi kwa wale waliomkamata. Aidha, Wananchi hao wamelalamikia  tabia ya baadhi ya watendaji kushindwa kutunza siri za watoa taarifa za kihalifu kwa kuogopa kutajwa na hivyo wananchi wengi kuhofia usalama wao na kushindwa kutoa taarifa za kihalifu.Wananchi hao pia wameomba Jeshi la Polisi kuwapatia mafunzo zaidi juu ya masuala ya ulinzi shirikishi,kujengewa kituo kidogo cha Polisi na pia Jeshi la Polisi kuongezewa vitendea kazi yakiwemo magari na pikipiki ili kurahisisha shughuli za usimamizi wa mara kwa mara


Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini


Kamishna wa  Operesheni na  Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi CP Awadhi Haji 



 

0 Comments:

Post a Comment