Subscribe Us

SERIKALI YAWATAKA WAFUGAJI WA KUKU KIJISAJILI

Serikali kupitia Bodi ya Nyama Tanzania imetoa rai kwa wafugaji wa kuku wa nyama Tanzania kujisajili kwenye Bodi hiyo ili kutambulika na kurasimisha biashara ili waweze  kupata fursa mbalimbali.


Hayo yamesemwa na Bi. Afsa Milandu Kaimu Meneja wa Idara ya Usajili na Udhibiti Ubora kutoka Bodi ya Nyama Tanzania wakati akifungua warsha ya siku moja ya wafugaji wa kuku wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa niaba ya Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. John Chasama. Warsha hiyo imefanyika Leo tarehe 09/06/2023 jijini Dar es Salaam.

Bi. Milandu amesema Wadau wa Ufugaji kuku wamekutanishwa kwenye warsha hiyo ili kuwapa elimu itakayowawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi Ubora.

"Tumewakutanisha ili kutoa elimu na pia kuwapa taarifa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika utakaofanyika mwezi Septemba. Elimu tuliyoitoa leo itawasaidia wafugaji wa kuku wa nyama kufahamu taratibu za  kusajiliwa na Bodi ya Nyama ili kutambulika na kuwezeshwa kupata mafunzo ili kuzalisha bidhaa bora na salama na kuzingatia vigezo vya ufugaji" amesema Bi. Milandu.

Bi. Milandu ameongeza kuwa  mfugaji aliyesajiliwa na Bodi ataweza kupata taarifa kuhusu masoko  au sehemu sahihi za kununua vifaranga vitakavyomzalishia bidhaa bora na kumwezesha mfugaji kuuza Nyama ya kuku iliyo salama.

Naye, Dkt. Mwajuma Chaurembo kutoka Ofisi ya Huduma za Magonjwa ya Mifugo (ZBC) amesisitiza kuwa ni wajibu wa mfugaji wa kuku kujisajili na kuhakikisha anapata kifaranga bora na kutoka kampuni gani ili kumwezesha pale anapopata changamoto kusaidiwa kirahisi na Bodi ya Nyama Tanzania.

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa kuku Tanzania Bw. Agusta Mrema ameishukuru Bodi ya Nyama Tanzania Kwa kuandaa warsha hiyo na kutoa rai kwa wafugaji wa kuku kujisajili ili kupata fursa na msaada hususan wa kisheria kutoka Bodi ya Nyama Tanzania pale wanapopata changamoto za kiufugaji.

Bw. Mrema amesema "Wadau wote tujiunge, tujisajili kwenye Bodi na vyama vya ufugaji ili tusipitwe na fursa kama hizi za kupatiwa elimu ya ufugaji.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Bodi ya Nyama Tanzania imehudhuriwa na wafugaji wa kuku zaidi ya 150 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.


0 Comments:

Post a Comment