Subscribe Us

TANZANIA, UINGEREZA KUIMARISHA USAWA WA KIJINSIA

 

Na WMJJWM, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekubaliana na Kamisheni ya Uingereza kushirikiana ili kuimarisha usawa wa kijinsia nchini.

Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Wizara na Kamisheni hiyo kilichofanyika jijini Dodoma Juni 7, 2023, kwa lengo la kutambulisha Programu na mkakati mpya wa kusaidia wanawake na wasichana kufikia ndoto zao (International Women and Girls strategy) utakaotekelezwa kati ya mwaka 2023 hadi 2030.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha elimu ya usawa wa kijinsia inatolewa kuanzia ngazi ya malezi ya awali huku akiwaomba wadau hao kuongeza ushirikiano kwenye maeneo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo wa Kamisheni ya Uingereza Nchini Kemi William, amebainisha kuwa, Kamisheni ipo tayari kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Programu za Elimu hasa mradi wa Shule Bora unaotekelezwa na Wizara ya Elimu kwa kuzingatia na kuhusisha makundi yote ndani ya jamii.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amekutana na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ambapo wamejadili ushirikiano bora wa kimaendeleo kwa lengo la kuwalinda Watoto na kuwawezesha wanawake na katika suala zima la utoaji wa elimu ya Afya ya uzazi kwa Wanawake na Wanaume ndani ya jamii.

Wakati wa Ziara hiyo, Kemi alifuatana na Wataalamu Waandamizi wa Elimu kutoka Kamisheni hiyo, Colin Bangay na John Lusingu.

MWISHO 



0 Comments:

Post a Comment