Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za Afya Bonanza ili waweze kupima afya zao na kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Senyamule ametoa wito huo Juni,14,2023 katika ufunguzi wa Bonanza la Afya Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika shule ya Msingi Chang’ombe na kufanikiwa jumla ya watu 721 hasa vijana kufikiwa na elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
“Nikipiga hesabu za haraka haraka ,tunategemea katika bonanza hili kufikia vijana 6000 katika mkoa wa Dodoma kwa kata 28,tumieni fursa kuja kushiriki bonanza hili ili kupata elimu ya afya kwa vijana na huduma zinazotolewa kwa Jiji la Dodoma ,na kila mmoja akielimisha kijana tutafikia vijana 30,000”amesema Senyamule.
Aidha,Mkuu huyo wa Mkoa amesema mada zinazotolewa ikiwemo elimu ya afya ya uzazi,lishe, ukatili wa Kijinsia ina umuhimu mkubwa katika makundi mbalimbali ya watu hususan Vijana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Watoto na Vijana kutoka Wizara ya Afya Dkt.Felix Bundala amesema kama Wizara wameamua kuwekeza nguvu zaidi kufikisha elimu ya afya na huduma kwa vijana ikiwemo namna ya kujikinga na UKIMWI na Mimba za Utotoni.
“Tumeamua kuangalia namna ya kufikisha elimu kwa vijana ikiwemo mimba za utotoni,ukatili wa kijinsia,Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza ,lishe ,Madhara ya dawa za kulevya,afya ya akili”amesema.
Mganga Mkuu Mkoa wa Dodoma Dkt.Best Magoma amesema Bonanza hilo litaleta tija kubwa kubwa kwa Vijana
Nao baadhi ya vijana wa Chang’ombe akiwemo Furaha David, Juma Athuman, pamoja na Mwajuma Hassan wamesema bonanza hilo limekuwa na manufaa makubwa kwao huku wakiiomba Wizara ya Afya kuendelea kuwezesha mabonanza kama hayo mara kwa mara .
“Kwa kweli kupitia bonanza hili la Afya nimeipongeza Wizara ya Afya kwanza imenipunguzia gharama Kwenda hospitalini lakini hapa vipimo nimepata bure na elimu ya afya imekuwa na msaada kwangu kujua namna cha kufanya”amesema Furaha David.
Ikumbukwe kuwa katika bonanza hilo la Afya mbali na utoaji wa elimu na huduma, michezo mbalimbali imefanyika kwa vijana ikiwemo mpira wa miguu,pete,kukimbiza kuku huku jumla ya watu 721 kata ya Chang’ombe wakifikiwa elimu ya afya kupitia bonanza hilo .
Kuhusu masuala ya lishe jumla ya watu 71 wamepimwa huku asilimia 15% wakigundulika kuwa na utapiamlo, 22% uzito uliozidi, magonjwa yasiyo ya kuambukiza jumla ya watu 68 wamepimwa ambapo Shinikizo la Juu la damu wamebainika watu watano(5),shinikizo la chini la damu wakibainika watu 2 na afya ya akili wakibainika watu watatu(3).
Katika ushauri nasaha jumla ya watu 66 wamepata ushauri nasaha na kuweza kupima Virusi vya UKIMWI ambapo hakuna hata mmoja aliyebainika kuwa na maambukizi huku katika suala la ukatili wa kijinsia(Gender Based Violence- GBV vilevile watu 66 wamepatiwa elimu hiyo huku mmoja akibainika kufanyiwa vitendo vya kikatili .
Halikadhalika, katika bonanza hilo la afya kupitia Wizara ya Afya ,Idara ya Huduma za Mzazi, Mama na Mtoto kwa kushirikiana na Elimu ya Afya kwa Umma,Ofisi ya Rais-TAMISEMI, chini ya uwezeshaji wa Mfuko wa Dunia( Global Fund) linafanyika katika mikoa mitano(5)halmashauri 18 lengo ni kufikia watu 15,000 katika mikoa hiyo,watu 833 kila Halmashauri na watu 208 katika kila kata .
Kwa mkoa wa Dodoma malengo ni kufikia watu 500 kila kata ambapo Kata ya Chang’ombe imevuka lengo na kufikia watu 721 na siku ya Juni 15.2023 bonanza litaendelea katika kata ya Kikuyu.
MWISHO.
Home »
» RC SENYAMULE VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA YA AFYA BONANZA KUPIMA AFYA ZAO.
0 Comments:
Post a Comment