Subscribe Us

WAZIRI WA ELIMU, PROF. MKENDA AMEWATAKA WAZAZI WENYE WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU KUWAPELEKA SHULE

Na WyEST Masasi, MTWARA Wito umetolewa kwa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kutowaficha watoto ndani badala yake wawapeleke shule kwa kuwa zipo shule maalum kwa ajili ya watoto hao. Hayo yamesemwa na Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipokuwa akizindua majengo mapya ya Shule Jumuishi ya Mfano ya Msingi Lukuledi iliyojengwa na Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Elimu na Kuendeleza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni kumnyima mtoto haki yake ya msingi ya kupata elimu. "Nipende kuwaasa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum popote nchini kutowaficha watoto ndani kwani Serikali iko tayari kuhakikisha watoto wote wanapata elimu stahiki," amefafanua Prof. Mkenda. Waziri Mkenda ameongeza kuwa katika mchakato unaoendelea wa mapitio ya Sera na mabadiliko ya mitaala, wanafunzi wenye mahitaji maalum wamepewa kipaumbele cha pekee katika kuhakikisha elimu wanayopata inawapa ujuzi kulingana na mahitaji waliyonayo pamoja na kuongeza walimu wenye taaluma hiyo. "Katika mchakato wa mapitio ya Sera na mabadiliko ya mitaala, suala la elimu jumuishi limetiliwa mkazo na tutaendelea kutilia mkazo hadi katika utekelezaji, ndio maana tunaendelea kuwekeza katika miundombinu stahiki kwao kwa kujenga shule jumuishi za Mfano na ninashukuru Benki ya Dunia kwa ufadhili wa mradi uliowezesha ujenzi huu sasa wanafunzi wetu wako katika mazingira bora ya kielimu," amesema Waziri Mkenda. Waziri Mkenda pia amewaasa wadau wa maendeleo kuendelea kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za Serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujifunzaji katika ngazi zote za elimu. Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Dkt. Magreth Matonya, Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema shule hiyo ni Jumuishi ikiwa na maana inachukua wanafunzi wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji maalum na kwamba awali ilikuwa katika majengo ambayo yalichakaa na finyu kulingana na idadi ya wanafunzi. Ameongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.4 na kwamba ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 320 kwa mara moja ambapo wanafunzi wenye mahitaji maalum watakaa bweni. Ametaja baadhi ya majengo yaliyopo kwenye shule hiyo kuwa ni mabweni 4, madarasa 12, ofisi 6, nyumba za watumishi 8, karakana 3, bwalo na jiko. Mengine ni jengo la Utawala, nyumba ya mkuu wa shule 1, matundu ya vyoo 9, na chumba cha maalum upimaji usikivu. Naye Mratibu wa Mradi wa ESPJ, waliofadhili mradi, Margaret Mussai amewataka walimu, wanafunzi na wanajumuiya wa shule hiyo kuhakikisha wanatunza miundombinu ya shule hiyo ili iweze kutumika mpaka vizazi vijavyo ikiwa kwenye hali nzuri. "Serikali imetumia fedha nyingi sana kujenga majengo haya hivyo niwaase walimu, wanafunzi na wanajumuiya wa shule hii kuitunza na kuienzi hii miundombinu ili itumike na kizazi cha sasa na cha baadae," amefafanua Mussai. Katika hafla hiyo Waziri Mkenda pia alikabidhi rasmi shule hiyo kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Abdalla Malela alipokea Hati ya Makabidhiano ya shule hiyo.
Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipokuwa akizindua majengo mapya ya Shule Jumuishi ya Mfano ya Msingi Lukuledi iliyojengwa na Wizara ya Elimu
Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi na viongozi wa Shule
majengo yaliyopo kwenye shule hiyo kuwa ni mabweni 4, madarasa 12, ofisi 6, nyumba za watumishi 8, karakana 3, bwalo na jiko.

0 Comments:

Post a Comment