Subscribe Us

SERIKALI IMETUTUPA,HAITUTAMBUI WANANCHI ZEPISA WATEMA NYONGO.

 
Na Moreen Rojas,
Dodoma.

Wananchi wa kijiji cha ZEPISA Dodoma jiji wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwatimizia huduma muhimu kama maji,umeme,miundombinu ya barabara pamoja na kituo cha afya.

Pendo Wilson ambaye ni mwanakijiji wa ZEPISA amesema kuwa maji yamekuwa changamoto kubwa kwao hadi kupelekea ndoa majumbani hazidumu kwani kina mama hutoka nyumbani saa 12 asubuhi hadi saa 2 usiku ambapo kisima kimechimbwa lakini hakuna kinachoendelea hali inayopelekea hata zahanati ya kijiji wahudumu kuondoka mapema hivyo wanaiomba serikali iwasaidie kwani vijiji vya karibu kama zaka kuna huduma zote lakini kwao zinashindwa kuwafikia pamoja na wanafunzi kukutana na changamoto ya barabara na maji shuleni hali inayopelekea usalama wa vyoo kuwa mdogo.

 Naye Yona Dickson ambaye ni katibu wa tawi  chama tawala(CCM)amesema kama kiongozi anapata wakati mgumu wa kuzungumza na wanakijiji kwani wanaona serikali iliyopo inaongea uongo na hakuna kinachotekelezwa kwani kijiji hicho kimesahaulika hivyo  wanaiomba serikali na viongozi wa ngazi za juu akiwemo Mbunge Mhe.Anthony Mavunde pamoja na Mkuu wa mkoa Mhe.Rosemary Senyamule wawakumbuke kwa kutembelea eneo husika ambapo kero kubwa ni miundombinu ya barabara kwani hakuna muunganiko mzuri kutoka ZEPISA mpaka hombolo bwawani.

"Miundombinu ya maji ni changamoto,kituo cha afya changamoto,miundombinu ya barabara changamoto,hospitali ya kijiji haina umeme tumeshachoka viongozi wanakuja wanaongea tu hakuna utekelezaji,wanasubiri karibia na uchaguzi tunawapigia kura baada ya miaka mitano hawaonekani kiukweli tumechoka na tunaomba serikali kama haitutambui tujue kwasababu haiwezekani kijiji hiki pekee ndio huduma muhimu hazifiki je sisi ni wakimbizi au watanzania?" Amehoji Ernest Mchano mwanakijiji Zepisa.

" Maji ndio kero ya kwanza kwani hakuna kabisa kina mama wanatoka asubuhi wanarudi saa sita usiku,kwa upande wa barabara kutoka mwaka 1972 barabara haieleweki licha ya TARURA kuja kuchonga barabara hali inayopelekea mvua ikinyesha kushindwa kutoka sehemu moja hadi nyingine,kuhusu suala la umeme hili nalo ndio tatizo kuu kwani hospitali ipo lakini hakuna umeme hali inayopelekea wahudumu kufanya kazi mchana tu na jioni wanaondoka na kusababisha kina mama kujifungulia njiani,na kwa upande wa shule changamoto kubwa ni vyoo vya wanafunzi ni shida tunamuomba Rais kuja kutembelea na kutatua kero hizi kwani sisi ni watanzania"Amesisitiza Mzee Emily Makasi Mwanakijiji na mwanaharakati wa kujitegemea.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ZEPISA B Ndugu.Musa Rashidi amesema ni kweli kero walizozisema wananchi zipo,vyoo mashuleni havitoshi na kumekuwa na ahadi bila matokeo kwani amekuwa akiwasiliana na viongozi husika bila matokeo chanya.

"Kama kiongozi na mwananchi naumia kuona toka kijiji hiki kianzishwe hakuna umeme wala hakuna vitendo vyovyote vinavyoendelea naiomba serikali itambue kwamba sisi tuko Dodoma jiji,ukitizama kwa upande wa visima kuna vya kiasili ambavyo havina uwezo wa kusambaza maji kote na tumekuwa tukifuatilia RUWASA bila kufua dafu na hali hii kama kiongozi inanikatisha tamaa kuona wananchi wangu hawafurahishwi na viongozi kushindwa kutekeleza majukumu yao kama walivyoahidi" Amesisitiza Mwenyekiti Zepisa B Ndugu Rashidi.

"Hakuna muunganiko kati ya serikali na viongozi wa chama ifike kipindi Serikali itambue kwamba kunawatu waliowachagua kwani kitendo cha kuto kututambua sisi inafika kipindi serikali ikiitisha mkutano wananchi hawafiki kwasababu wanachoka kudanganywa,hakuna huduma zozote muhimu wakati tupo Dodoma jiji na Zepisa inafahamika na Serikali na kama haifahamiki basi watutafutie sehemu ya kutupeleka" Ameongeza Abi Mwanza mwanakijiji Zepisa.

Naye Ndugu Daudi Kamunya ambae ni mwenyekiti wa ZEPISA A amesema kuwa umeme kwenye kituo cha afya Zahanati bado ni changamoto kwani huwezi kufanya kazi bila umeme,hivyo amewaomba wananchi kuwa wa pole kusuburi huduma hiyo kwani changamoto ya umeme iko mbioni kutatuliwa.










0 Comments:

Post a Comment