Subscribe Us

MADEREVA WA MALORI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI MAAMBUKIZI YA VVU

 

Na Mwandishi wetu- Singida

Madereva wa magari yaendayo masafa    marefu ndani ya ndani na nje  Nchi wamehimizwa  kuchukua tahadhari dhdi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI wakati wote wanaofanya shughuli zao za usafirishaji pamoja na kujenga utamaduni wa kupima afya zao ili kuanza matumizi ya dawa  mapema pindi watakapogundulika kuwa na maambukizi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga  wakati akizungumza na madereva wa malori  wanaoegesha malori hayo katika Kijiji cha Majengo, pamoja na kukagua Kituo cha Maarifa ya UKIMWI Halimashauri ya Wilaya ya Manyoni  mkoani Singida akiwa ameambatana  na  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI .

Mhe. Ummy amesema lengo la  kufika  katika kituo hicho ni kuzungumza na madereva hao akisema wako katika hatari  kubwa ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Kutokana na shughuli zao za masafa marefu pamoja na kukagua huduma za kiafya zinazotolewa kituoni hapo.

“Nipende kuwakumbusha na kuwasisitiza mjitokeze mpime afya zenu ili mjue mko katika hali gani, tunatambua kulingana na kazi zenu mnatembea umbali mrefu na mnaenda  maeneo mengi kama mikoani na nje ya Nchi kwahiyo mko hatarini  kupata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na niwaombe mtumie kituo hiki cha Maarifa kupata elimu ya UKIMWI na magonjwa mengine ili muwe salama,” Amesema Mhe. Ummy.

Aidha Naibu Waziri huyo amewakumbusha kuendelea na matumizi ya dawa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIWMI ili kuimarisha kinga ya mwili , kujiepusha na magonjwa nyemelezi ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa imara kiafya huku akiissisitiza  jamii kutowanyanyapaa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI na badala yake kuwaonyesha upendo, kuwajali  na kuwashirikisha katika maendeleo.

Aidha akisoma taarifa ya Kituo hicho mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Dkt. Ainea Mlewa  amebainisha kuwa hali ya upimaji kuanzia  mwezi Julai 2022 hadi Septemba 2023 jumla ya  madereva wa malori waliojitokeza kupima  maambukizi ya VVU ni 684 waliogundulika na maambukizi  wakiwa ni 19 kati yao 15 ni wanawake  wakati wanaume wakiwa ni wanne ambapo waliunganishwa katika Kliniki ya tiba na mafunzo.

 “Malengo ya mradi ni kuhamasisha wananchi kupima bila uoga, kutoa ushauri, kuhamasisha upimaji wa VVU kwa  hiari, kuhamasisha upimaji kwa kutumia ushawishi wa mtoa wa huduma, kutoa elimu ya UKIMWI pamoja na matibabu ya magonjwa ya zinaa, kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kugawa kinga na elimu ya matumizi  yake, elimu kwa vikundi vya WAVIU na elimu sahihi ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU,” Amefafanua Dkt. Mlewa.

=MWISHO=

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akisalimiana na baadhi ya wataalam wa afya katika Kituo cha Maarifa ya UKIMWI kilichopo Kijiji ch majengo, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida alipowasili kituoni hapo akiwa na   Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI tarehe 10 Oktoba, 2023.   

 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza na baadhi ya Madereva wa  Malori  wanaoegesha Malori yao katika Kijiji cha Majengo , Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida akiwa pamoja na   Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI tarehe 10 Oktoba 2023.


Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Dkt. Ainea  Mlewa akitoa taarifa ya  Kituo cha Maarifa ya UKIMWI kilichopo Kijiji cha Majengo , Halmashuri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida  mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI ambaye pia ni Mbunge Viti Maalumu  Mhe. Juliana Shonza (wa pili kulia) akiuliza swali wakati wa ziara ya Kamati hiyo ilipotembelea Kituo cha Maarifa ya UKUMWI kilichopo KIjiji cha Mjengo, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida tarehe 10 Oktoba, 2023.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)


 

0 Comments:

Post a Comment