Subscribe Us

UBORA WA HUDUMA ZA AFYA UNACHANGIWA NA WAKUNGA NA WAUGUZI.

Na Moreen Rojas,

Dodoma.



Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema asilimia 60 ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanatoka  kada za uuguzi na ukunga hivyo kuchangia ubora wa huduma  zinazotolewa katika Hospitali na Vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Mollel amebainisha hayo Machi 18, 2024 wakati wa kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa utendaji kazi wa utoaji wa huduma za uuguzi na Ukunga zoezi lililoenda sambamba na uzinduzi wa jarida la idara ya Uuguzi na Ukunga jijini Dodoma.

Dkt. Mollel amesema kada ya Uuguzi imekuwa muhimu katika kutoa huduma bora kwa sababu asilimia 80 ya kazi za afya zinatekelezwa na kada hiyo na kutoa rai kada hiyo kujumuishwa kwenye mfumo wa utoaji wa maamuzi.

“Ukiona kituo cha afya kinatoa huduna bora ni kwa sababu ya uwepo wa wauguzi ambao ndio wamekuwa watendaji wakuu ambao wanakaa muda mwingi na wagonjwa hivyo ni muhimu wakawekwa kwenye mfumo wa uongozi na utoaji wa maamuzi na uundwaji wa sera”. Amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel Ameongeza kuwa wauguzi na wakunga wanapopata fursa ya kuingia ndani ya mfumo wa uongozi watasaidia kuhakikisha mambo yanaboreshwa kwenye sekta ya Afya lakini pia maslahi yao.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sella ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuajiri Wauguzi na Wakunga zaidi ya 40,000 kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 na kuongeza kuwa  kada hiyo ina dhamana kubwa katika utoaji wa huduma hivyo wazingatie miongozo, kanuni na sheria zilizowekwa kwa maslahi ya taifa.

“Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri wauguzi na wakunga zaidi ya elfu arobaini hii inaonyesha umuhimu na dhamana ya kada hii kwa sababu hawa ndio hutumia muda mwingi kukaa na wagonjwa.

Kikao hicho kilichowakutanisha Viongozi wauguzi na Ukunga kote nchini kimebeba kauli Mbiu isemayo “Huduma Staha na Mawasiliano ni Wajibu wa Kila Mtoa Huduma za Afya”.




0 Comments:

Post a Comment