DODOMA
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Ajira na Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ally Msaki ameshauri Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Dodoma (SIDO) kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na vijana zinakuwa na ubora.
Msaki ameyasema hayo Aprili 25, 2023 SIDO Dodoma kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 147 na kukabidhi vifaa vilivyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Ujerumani GIZ.
Amewataka vijana kutumia ujuzi walioupata kuzalisha bidhaa zenye ubora unaohitajika katika soko la kitaifa na kimataifa.
Msaki amesema kwa Mwaka 2022/23 serikali imetenga Sh.Bilioni tisa ili kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ujuzi katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
"Jukumu la serikali ni kuhakikisha kunakuwepo sera na mipango ya kuwaongoza vijana ili wajiajiri, kuweka miundombinu sahihi ya kuwawezesha vijana kufanya shughuli za kiuchumi na kuhamasisha wadau kuhakikisha vijana wanafanya shughuli za kiuchumi,” amesema.
Naye, Meneja wa Mradi wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kimataifa (FIC), Erustus Ouko amesema lengo la mradi huo ni kushirikiana na serikali katika kusaidia kukuza ajira kwa vijana na wanawake.
Awali, Meneja wa Mradi wa Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ), Awadhi Milasi, amesema shirika hilo limechangia vifaa vyenye thamani ya Sh.Milioni 34 ili kufanikisha malengo ya SIDO Dodoma hususani kuwainua wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi wa SIDO Dodoma, Sempeho Manongi amesema vijana 147 kati ya 151 waliosajiliwa wamehitimu mafunzo yao huku baadhi wakishindwa kuhitimu kwa sababu mbalimbali.
Mmoja wa Wanufaika wa mafunzo hayo, Anthon Makasi amesema amepata ujuzi ambao hakuwa nao awali na kutoka kuwa mjasiriamali mdogo hadi kuwa mkubwa na anatarajia kujiajiri baada ya mafunzo hayo.Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Ajira na Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ally Msaki
Akikabidhi cheti kwa Muhitimu wa uanagezi
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Ajira na Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ally Msaki Akikagua Bidhaa za wajasiriamali
0 Comments:
Post a Comment