Subscribe Us

YALIYOJIRI LEO AGOSTI 15, 2023 WAKATI WA UFUNGUZI WA JENGO LA KITEGA UCHUMI (SAFINA HOUSE) LA KANISA LA ANGLIKANA*


*Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan*

#Pamoja na kutoa huduma zilizopangwa, jengo hili la kitega uchumi limebadili mandhari na limeleta mandhari ya kupendeza ndani ya Jiji la Dodoma, nawapongeza kwa kukamilisha mradi huu.

#Jengo hili ni la kitega uchumi, hivyo linaashiria kukua kwa shughuli za kiuchumi za Kanisa la Anglikana, Serikali imefurahishwa na kukamilika kwa mradi huu kwa kuwa utachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

#Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi pamoja na mashirika ya kidini nchini, mbali na kutoa huduma za kiroho, taasisi hizi zinasaidia Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.

#Jukumu la kilimo ni jukumu kubwa, mnalibeba na mnaisaidia sana Serikali kwani suala la kilimo na chakula ni miongoni mwa ajenda kuu za Serikali.
 
#Kanisa limekuwa likiwajali watoto wenye mahitaji mbalimbali, wajane na masikini wasiojiweza, huu ndio utumishi mwema na wito mkuu wa kanisa, natumia fursa hii kulipongeza kanisa Anglikana kwa kazi hizi.

#Pamoja na kazi kubwa mnayoifanya, nawahimiza kazi ya kulinda maadili na kukemea maovu, kuwafundisha vijana pamoja na watu wazima wale ambao wanalitumia kanisa kufanya mambo ya hovyo.

#Nawapongeza Kanisa la Anglikana kwa kufungua jengo hili la kitega uchumi ambalo ni la aina yake kwa usanifu na muonekano wake. Natoa pongezi za dhati kwa ubunifu mkubwa.

#Serikali itaendelea kutambua na kuenzi mchango wa Kanisa Anglikana Tanzania pamoja na kudumisha ushirikiano wa karibu na kanisa hili pamoja na taasisi zote za kidini nchini kwani tukifanya kazi kwa pamoja tutaweza kuongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa letu.

#Natoa wito kwa Kanisa kuendelea kuwahimiza waumini wenu kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma, tunataka maendeleo ya Dayosisi hii yaende sambamba na maendeleo ya jiji na mkoa wetu wa Dodoma.

#Nawasihi viongozi wa kanisa hili na viongozi wote wa dini nchini kuendelea kuliweka taifa letu katika mikono salama ya Mwenyezi Mungu ili lidumu katika amani, umoja na mshikamano, kamwe tusikubali kuyumbishwa na mtu yeyote asiyelitakia taifa letu mema

*Aliyosema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule*

#Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan umetufundisha kushirikiana, kuheshimu watu na kuheshimiana pamoja na kuthamini watu wengine bila kujali kabila, dini, itikadi za kisiasa wala chochote, tumeshuhudia wewe ukishirikiana na kila mtu kwa vitendo jambo hili ni funzo kubwa kwetu.

#Sisi Mkoa wa Dodoma tumepokea maelekezo yale ambayo tumeyaona kwako kwa vitendo kwa kushirikiana na taasisi zote za dini na makundi yote kama ambavyo umeelekeza.

#Nawashukuru viongozi wa dini kwa Mkoa wa Dodoma ambavyo wanashirikiana na mkoa na wilaya zote na kufanya amani na utulivu kwa mkoa huu kuendelea kuimarika.

#Nakupongeza na kukushukuru Rais Samia kwa kuleta miongozo ya Serikali na kuonesha utashi wa dhati kwa kuonesha fursa za uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya matamanio ya kila mtu kuwekeza nchini.

#Kanisa la Anglikana wamekuwa wadau wazuri  kwa kuwekeza ambapo leo umeufungulia jengo kubwa la uwekezaji, kanisa hili pia wana miradi ya elimu, hospitali ya macho.

#Ufunguzi wa jengo hili ni kitega uchumi kikubwa ambacho kitaenda kutupambia na kutuongezea sifa na hadhi ya Mji wa Dodoma.

*Aliyosema Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Dkt. Chilongani Dickson*

#Tunakushukuru Rais, Mhe. Samia kwa kujumuika nasi katika tukio hili, ujio wako unaendelea kuthibitisha kwamba wewe ni Rais unaewajali na kuwatumikia Watanzania wa dini zote, makabila, rangi na itikadi  zote. Ingawa Serikali haina dini, wananchi wake wana dini na Serikali inaziheshimu dini zote na inashiriki katika matukio mbalimbali ya dini.

#Nakupongeza Rais Samia kwa uongozi wako mahiri na kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya wewe na Serikali yako katika Awamu ya Sita kwa maendeleo ya nchi yetu na kwa ustawi wa wananchi wote, tangu umepokea kijiti cha uongozi wa Taifa letu, hujayumba wala kutetereka.

*Aliyosema Askofu Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Mha. Dkt. Maimbo Mndolwa*

#Kanisa halifanyi kazi za injili pekee bali linafanya na kazi za maendeleo na za kijamii, hayo yote tunayafanya tukijua ya kwamba mkono wa Mungu unagusa watu kwa njia nyingi na moja ya sababu ya kufanya haya ni kugusa maisha ya watu wenye uhitaji mkubwa.

#Nawatia moyo Maaskofu kuwa kazi mnayofanya pamoja na maumivu na maneno mengi, Mungu anaona, pasipo na kusemwa hakuna kufanya kazi na palipo na kazi yenye nguvu lazima maneno yatainuka na siku zote ushindi utainuka pale tunaposimama na Mungu.

#Pamoja na changamoto zilizoikumba Dunia kutokana na changamoto za UVIKO-19 na nyinginezo, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi, sisi waumini wa Kanisa Anglikana Tanzania tunakuombea mchana na usiku.

#Suala la kuamuru wanawake kuwa Wachungaji limekuwa na mjadala ndani ya Kanisa Anglikana na maamuzi yamekuwa ni kuiachia Dayosisi husika kuamua kama zinataka kufanya hivyo au laa. Dayosisi ya Central Tanganyika ndio Dayosisi ya kwanza Tanzania kuanza kuwapa huduma Wachungaji wanawake ambapo hadi sasa Dayosisi hii ina jumla ya Wachungaji wanawake 65.

#Dayosisi hii inajishughulisha pia na huduma za elimu, afya na jamii ikiwemo hospitali, shule za sekondari, chuo kikuu cha St. John na Chuo cha Ualimu kilichopo Muleba, Kagera.

#Dayosisi ina shule 9, kati yake mbili ni za msingi (english medium), shule mbili za sekondari na shule moja ya kimataifa inayotumia mtaala wa cambridge, tumeanzisha shule ya ufundi ya viziwi kwa kutumia lugha ya alama, shule ya msingi ya wasioona, wenye uono hafifu na walemavu wa ngozi.

#Naishukuru Serikali kwa msaada ambao inaendelea kuutoa kwa watoto waliopo katika shule hizo ikiwemo Walimu, chakula na vitabu vya kufundishia.

#Kwa kipindi cha takriban miaka 10, Dayosisi imeweza kusomesha watoto yatima takriban 7,000 kwa ngazi ya shule ya msingi, sekondari, elimu ya ufundi na vyuo vikuu kwa kuwapatia lishe bora, vifaa na sare za shule, kuwalipia ada na matibabu.

#Dayosisi imewachimbia visima na kuwajengea matenki ya maji wananchi wa wilaya za Bahi na Chamwino pia ina kituo cha afya na hospitali mbili pamoja na Taasisi ya Afya na Sayansi ya Mvumi.

#Ujenzi wa jengo hili la kitega uchumi ulianza mwaka 2017, hadi kukamilika kwa jengo hili, tumetumia shilingi bilioni 8 ambapo katika hizo, shilingi bilioni mbili ni msaada kutoka kwa marafiki zetu wa Trinity Church Wallstreet Newyork, shilingi bilioni tatu ni fedha zetu za ndani na bilioni tatu ni mkopo kutoka benki.

#Jengo hili tayari lina wapangaji wa kuaminika na litaliingiza Dayosisi takriban shilingi bilioni moja kwa mwaka, kwa kutumia mapato haya na jitihada zetu za ndani ni dhahiri kwamba mkopo huu tutaulipa kwa kipindi kifupi.

#Tunataka jengo hili lilete taswira ya kanisa kuendelea kujikomboa kiuchumi na hatimaye liweze kujitegemea kwani kwa muda mrefu kanisa limeendelea kutegemea misaada wakati nchi yetu ina fursa nyingi na rasilimali za kutosha.

#Jengo hili lina ukumbi unaoingiza takriban watu 400, tumejenga ukumbi huu ili kuwa na sehemu ambayo itawaleta vijana wa dini zote ili kuwapatia mada mbalimbali na kuwapa fursa za wao kubadilishana mawazo ya kijamii, kiuchumi na maadili ya kitanzania.

*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*


0 Comments:

Post a Comment