Home »
» MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA AMETOA MAELEZO KUHUSU AJALI YA NDEGE
MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA AMETOA MAELEZO KUHUSU AJALI YA NDEGE
*YALIYOJIRI LEO NOVEMBA 14, 2022 WAKATI MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI - MAELEZO NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA AKITOA TAARIFA YA MAELEKEZO YA BARAZA LA MAWAZIRI KUHUSU AJALI YA NDEGE YA KAMPUNI YA PRECISION AIR ILIYOTOKEA NOVEMBA 6, 2022*
#Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika leo Novemba 14, 2022 jijini Dodoma kimepokea taarifa ya awali ya ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision Air iliyotokea mnamo Novemba 6, 2022 na hatua zilizochukuliwa baada ya ajali.
#Baraza la Mawaziri limewaelekeza Wataalam wa ndani kushirikiana na Wataalam kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi kuhusiana na ajali hii ili kupata chanzo cha ajali na kutoa mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa mara baada ya ajali kutokea.
#Baraza la Mawaziri limetoa maelekezo haya kwa kuzingatia kwamba nchi yetu imesaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mara baada ya ajali ya anga kutokea.
#Baraza la Mawaziri pia limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe kwa namna mbalimbali ambazo zitatuwezesha sisi kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulionao sasa katika kukabiliana na majanga pale yanapotokea.
#Ajali za ndege zinapotokea, zipo hatua tatu zinazofuatwa katika uchunguzi ikianza na timu ya uchunguzi ya ajali ya ndege ambayo inafanya uchunguzi wake na kutoa maelezo ya awali ndani ya siku 14, inafuatiwa na ripoti ya awali ambayo inatolewa ndani ya siku 30 na tutamaliza na ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea, hatua hizi zote tayari zimeshaanza.
#Serikali inawaomba wananchi wote kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi huu unafanyika na baada ya uchunguzi kukamilika wananchi watajulishwa.
#Baraza la Mawaziri linawashukuru na kuwapongeza Wananchi na wote waliohusika katika uokozi baada ya ajali hii kutokea.
#Maeneo ya uchunguzi yote yanaainishwa na timu za wachunguzi, taratibu zote za kimataifa ambazo zinaelekeza juu ya maeneo yanayopaswa kufanyiwa uchunguzi zinazingatiwa.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*
0 Comments:
Post a Comment