Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewataka uongozi wa Wilaya na Chuo cha Ufundi stadi VETA Bahi kuhakikisha wanatengeneza historia nzuri ya chuo hicho ili kilete matokeo chanya na kiwanufaishe watu mbalimbali hususani wakazi wa wilaya hiyo na watu/ wanafunzi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Hayo yamesemwa mapema hii leo Februari 20/2024 na Mhe. Senyamule wakati alipofanya uzinduzi/ ufunguzi wa mafunzo ya ufundi stadi yaliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Chakula la Chuo hicho wakati akizungumza na wanafunzi, Walimu na wadau mbalimbali waliojitokeza katika uzinduzi wa mafunzo hayo.
“Ufundi ni Ubunifu na kusoma bila vitendo bado hujawa fundi mahili sasa ili kufikia malengo ni lazima kuwa wabunifu na msome kwa vitendo ili muwe bora Zaidi na tengenezeni Misingi mizuri ya chuo chenu ili kiwe mfano wa kuigwa kwa wilaya yenu, Mkoa na Taifa kwa Ujumla na kupitia misingi mtakayoitengeneza mtakua mmeifaharisha Dodoma“,amesema Senyamule.
Naye Kaimu Msajili wa Chuo hicho Bw.Daudi J. Lyanga ameweka bayana ukubwa wa chuo hicho kuwa kina takribani hekari 52 ambazo zilitolewa na wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo na hadi sasa kimekamilika Katika hatua ya ujenzi na tayari kimeanza kutoa mafunzo.
Miongoni Mwa kozi zinazotolewa katika chuo hicho ni Ufundi ujenzi, uchomeleaji vyuma, Ushonaji, Uhazili na kompyuta,ufundi umeme wa majumbani na ufundi magari ambapo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 66 wamepokelewa chuoni hapo.
Awali katika kuendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuhakikisha Dodoma inakua ya kijani Mhe. Senyamule akifuatana na viongozi wa ngazi mbalimbali wamepata fursa ya kupanda miti katika maeneo yanayozunguka chuo hicho.
MATUKIO YA PICHA Mhe. Senyamule WAKATI ALIPOFANYA UZINDUZI /UFUNGUZI WA MAFUNZO YA UFUNDI STADI
0 Comments:
Post a Comment