Subscribe Us

WASTANI WA MATUMIZI KWA SIKU KWA MTU NI SHILINGI 1,419.

 
Na Moreen Rojas,
Dodoma.


Matokeo yameonesha kuwa katika kaya za Walengwa, wastani wa matumizi kwa siku kwa mtu ni TZS 1,419 (sawa na US$0.6 kwa siku) kwa mwaka 2022, ambapo kiwango hicho kipo chini ya mstari wa umaskini wa Tanzania Bara wa TZS 1,859 (US$0.80) kwa mwaka 2022.

Hayo yameelezwa na Mhe.George Simbachawene Waziri wa Nchi,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora wakati akizindua ripoti ya awali ya kutathimini kipindi cha pili cha mpango wa kunusuru kaya maskini Tanzania 2022 uliofanyika katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.

Aidha ameongeza kuwa matokeo yanaonesha pia kuwa, wastani wa matumizi ya kaya moja ya Mlengwa kwa mwezi ni TZS 152,621 (US$65.50), ambapo matumizi ya chakula yanachukuwa nafasi kubwa kwa TZS 113,256 (US$48.6), sawa na asilimia 74.2 ya matumizi yote ya kaya.  Kiwango hiki cha matumizi ya kaya za Walengwa kwa mwezi kipo chini ukilinganisha na wastani wa matumizi ya Kaya moja kwa mwezi Nchini Tanzania.


"Kwa msingi wa matokeo haya ni dhahiri kuwa Walengwa katika Mpango wa TASAF matumizi yao yanatumika zaidi kwenye huduma za chakula badala ya kuwekeza kwenye shughuli za uzalishaji ili kuongeza mtaji na kutoka katika hali ya umaskini iliyopo kwa sasa, kwa msingi huo, Serikali itaelekeza nguvu zaidi katika kaya hizi na kuhamasisha Walengwa kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji kwa lengo la kujiongezea kipato na hatimae kutoka katika Umaskini uliokithiri" Amesema Simbachawene


Aidha ameongeza kuwa kama tunavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ilianzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) ili kupunguza umaskini uliokithiri (Extreme Poverty) na kuondoa mwendelezo wa umaskini kwa vizazi vijavyo.

"Mpango huu unalenga kuimarisha hali za maisha ya Kaya za Walengwa kiuchumi na kijamii kwa kuziwezesha kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji ya msingi,ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa, Mpango wa TASAF unatoa ruzuku kwa Kaya za Walengwa zinazopaswa kutimiza masharti yaliyoainishwa katika maeneo ya huduma za jamii, kiuchumi na mazingira wanayoishi"


"Napenda nizungumzie kuhusu shughuli za kiuchumi za Kaya za Walengwa wa Mpango, matokeo yanaonesha kuwa, katika shughuli za uzalishaji, asilimia 50 ya Kaya za walengwa zinajishughulisha na kazi za shamba la familia, asilimia 22 zinafanya kazi za malipo, na asilimia 15 wamejiajiri wenyewe,takriban asilimia 57 ya chakula katika Kaya za Walengwa huzalishwa na kaya zenyewe kwa matumizi yao wenyewe au kupewa zawadi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki na asilimia 43 iliyobaki ya chakula hununuliwa, kwa matokeo haya napenda kuhamasisha Walengwa wa Mpango wa TASAF kuhakikisha wanazalisha chakula kwa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali au wadau wengine katika maeneo wanayoishi, kwa sasa mvua zinazoendelea kunyesha Nchi nzima sote tutumie fursa ya kuotesha mazao ya muda mfupi kama mboga za majani, mahindi na mazao mengine kwa lengo la kujiongezea kipato"Amesisitiza Mhe.Simbachawene


Aidha mwaka 2024 TASAF itafanyika tathmini ya pili kwa lengo la kufuatilia na kutathimini malengo yalibainishwa katika Mpango unawahusisha Walengwa 5,146,720.


"Tathmini hii ya awali imekusanya taarifa za kaya na wanakaya zinazohusu hali ya elimu; afya; uwezeshaji wa wanawake; matumizi na usalama wa chakula; namna ya kukabiliana na majanga katika kaya; makazi na rasilimali za kaya; shughuli za kaya zisizokuwa za kilimo; akiba na mikopo; ajira na matumizi ya muda; shughuli za kilimo na mifugo; na unyanyasaji wa kijinsia,taarifa hizi zote ni za msingi katika kutoa viashiria vya hali ya umaskini katika kaya" Ameongeza Mhe.Simbachawene


Kwa upande wa Hali ya Makazi, matokeo yanaonesha kuwa, Kaya za Walengwa zinaishi katika mazingira yasiyoridhisha,asilimia 38 ya Kaya za Walengwa kuta za nyumba zimejengwa kwa udongo.


"Hapa niagize TASAF na viongozi wengine katika ngazi ya kata, Kijiji na kitongoji kufuatilia kwa karibu mazingira wanayoishi hawa ndugu zetu na kuweza kutoa ushauri wa kutosha wa namna ya kujenga kwa gharama nafuu na kutumia vyombo vingine vya Serikali kama Shirika la Nyumba la Taifa,nchi nyingine katika Bara la Afrika na duniani kote kundi hili hupewa kipaumbele katika makazi wanayoishi,serikali italifanyia kazi katika mpango mwingine unaofuata ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuwaweka hawa walengwa katika mazingira mazuri zaidi"Amesisitiza Mhe.Simbachawene


 

0 Comments:

Post a Comment