Ni Kufuatia Changamoto za tozo za Halmashauri zilizowasilishwa na wachimbaji Morogoro
Waziri Mavunde awapongeza Morogoro kuvuka lengo la makusanyo ya maduhuli
Serikali kuongeza nguvu ya Utafiti Morogoro
Wachimbaji wamshukuru Rais Samia kwa mashine za uchorongaji
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Wizara ya Madini imekubaliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kukutana na kutatua changamoto ya tozo zinazowekwa na Halmashauri kwa wachimbaji wa madini nchini.
Aliyasema hayo Agosti 5, 2024 Mkoani Morogoro wakati wa kikao na Wachimbaji wa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji mkoani hapa.
“Nimesikiliza kwa umakini mkubwa kilio hiki cha tozo za Halmashauri na tozo nyinginezo kwa wachimbaji wadogo,kero hizi sio hapa tu zipo maeneo yote nchini," alisema Mavunde.
Aliongeza kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa kuzitaka Wizara hizo mbili kukutana ili kushughulikia suala hilo.
"Nataka niwahakikishe mimi na Mwenzangu Mhe. Mohamed Mchengerwa tumekubaliana kwamba mara baada ya ziara ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu mkoani Morogoro tutaitisha kikao cha pamoja ili kushughulikia suala hili,".
Pia, Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wachimbaji wa Morogoro kuhusu dhamira ya Rais Dkt. Hassan kuongeza nguvu kwenye eneo la utafiti wa madini ikiwemo Mkoa Morogoro kunufaika.
Mhe. Mavunde aliipongeza Ofisi ya Madini Mkoa wa Morogoro kwa kuvuka lengo la ukusanyaji maduhuli kufikia shilingi bilioni 4.9 zaidi ya lengo lililowekwa la shilingi bilioni 4.2bn.
Akisoma risala kwa niaba ya wachimbaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Morogoro(MOREMA) Dkt. Omar Mzeru, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mashine za uchorongaji kwa wachimbaji wadogo na kutumia fursa hiyo kumuomba Waziri wa Madini kushughulikia changamoto kubwa inayotokana na uwepo wa tozo nyingi zinatozwa na Halmashauri na Taasisi nyingine za Serikali kwakuwa zimekuwa zikiwarudisha nyuma kimapato wachimbaji wadogo.
0 Comments:
Post a Comment